SERIKALI YAMJIBU MBOWE DARAJA LA WAMI....UJENZI KUGHARIMU BILIONI 67.8



Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eliasi Kwandikwa ameliambia Bunge leo Ijumaa Novemba 9, 2018 kuwa mkandarasi Power Construction Corporation kutoka China amekwisha saini mkataba toka Juni 28, 2018.
Kwandika ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe ambaye hakuwepo na swali hilo liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini.

Mbowe ametaka kujua Daraja la Wami lilijengwa mwaka gani na kama Serikali haioni ajali zilizotokea hapo zinatokana na wembamba wa daraja na kuna mpango wa kupanua daraja hili sambamba na eneo lote la barabara la mteremko wa mto huo.

"Daraja la Wami lenye urefu wa mita 88.75 lililoko mkoa wa Pwani lilijengwa mwaka 1959 na ndicho kiungo cha kutoka Chalinze kwenda ukanda wa Kaskazini," amesema Kwandikwa

Amesema daraja hilo jipya litakuwa na urefu wa mita 513.5 na upana wa mita 11.85 na litajengwa umbali wa mita 670 pembeni mwa daraja la zamani.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, kazi ya ujenzi wa daraja hilo utakuwa wa miezi 24 na litagharimu Sh67.8 bilioni.

Chanzo:Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527