Tuesday, November 27, 2018

MADEREVA WA MABASI WAGOMA BUKOBA WAKIPINGA USHURU

  Malunde       Tuesday, November 27, 2018

Abiria waliopaswa kusafiri kutoka manispaa ya Bukoba kwenda katika wilaya mbalimbali mkoani Kagera  leo wameshindwa kusafiri, kutokana na madereva kugoma wakipinga kupandishiwa ushuru katika kituo kikuu cha mabasi.

Baadhi ya madereva  wamesema hawakubaliani na hatua hiyo kwa sababu hakuna kilichoboreshwa katika kituo hicho ambacho hakina vyoo, nyumba ya kupumzikia abiria na kimejaa vumbi hali inayowasababishia adha kubwa hasa kipindi mvua zinaponyesha.

“Kama wanataka kupandisha ushuru basi waboreshe Stendi kwanza ili tuone mapato wanayokushanya kuwa yanafanya kazi” alisema Paskates Paschale.

Mafutah Rajab ambaye pia ni dereva alisema haifai wao kupandishiwa ushuru wakati nauli ya abiria bado ni ile ile tangu mwaka 2013, na kuwa mwaka huo walikuwa wakinunua mafuta kwa shilingi 1,750 lakini sasa wananunua kwa shilingi 2,600 kwa lita moja.

Naye William Wilbard alisema  hawakushirikishwa katika mchakato mzima wa kupandisha ushuru, na kuwa wao wakiwa katika kituo hicho cha mabasi walisikia gari likipita linatangaza kuwa ushuru wa kuondoa gari katika kituo hicho umepanda.

Baadhi ya abiria waliokutwa wamekaa katika magari wakiwa na matumaini ya kusafiri waliomba serikali kuwasiliana na wadau wote wanaohusika na kukaa nao kikao ili kupata maamuzi ya pamoja, kuliko serikali kukaa na kuamua na matokeo yake wanaoumia ni abiria.

“Mimi naumwa, nilipaswa nisafiri kwenda Kyaka nikapumzike, lakini nimefika Stendi sijui kinachoendelea nikapanda gari lakini tangu nimepanda hadi sasa gari haliondoki, ndiyo nakuja kuambiwa kuna mgomo” alisema bibi Reocadia Petro. 

Mwenyekiti wa Chama Cha Kutetea Abiria Bashiru Samadu aliwataka wahusika wote kukaa meza moja na kupata muafaka maana wanaoumia ni abiria, ambao wamefika kituoni hapo wakiwa na matumaini ya kusafiri lakini wakakuta kuna mgomo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba Richard Mihayo aliwataka madereva kuendelea kulipa kiwango kipya cha shilingi 2,000 kwa Hiace na shilingi 4,000 kwa Coaster kila wanapotoka katika kituo hicho, na kuwa uongozi wa manispaa utaendelea kufanyia kazi changamoto nyingine.

“Sheria hii ilipitishwa tangu mwaka 2005 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2008, inawezekana wengi wa wanaolalamika sasa wakati huo hawakuwepo, kinachofanyika hivi sasa ni utekelezaji wa sheria hii”, alisema Mihayo.

Hata hivyo kauli hiyo ilipingwa na madereva waliokuwa wakimsikiliza na hatimaye wakakubaliana kwenda kufanya mazungumzo na kupata muafaka kuhusiana na suala hilo.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post