Picha : TAASISI YA IMETOSHA YATOA MSAADA KWA MWENYE UALBINO ALIYEPATA UPOFU WA MACHO SHINYANGA

Taasisi ya Imetosha ya Jijini Dar es salaam imemtembelea na kumpatia msaada bwana Charles Kulwa Jagadi (41) mwenye Ualbino mkazi wa kijiji cha Mhunze kata ya Kishapu wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambaye amepata upofu wa macho kutokana na ugonjwa wa saratani ya macho unaomsumbua uliopelekea jicho moja kung’olewa.

Mtendaji Mkuu wa Imetosha Foundation,Henry Mdimu aliyefika nyumbani kwa Jagadi leo Jumapili Novemba 11,2018 amesema taasisi yake imeguswa na hali ngumu ya maisha anayopitia Jagadi hivyo kuamua kumjengea kibanda cha kufanyia biashara ya mkaa ili kumsaidia katika maisha yake.

Alisema Imetosha Foundation kwa kushirikiana na Dar Marathon Club ya jijini Dar es salaam wameamua kuchangishana fedha kwa ajili ya kumsaidia Jagadi ili aweze kuendesha familia yake yenye watoto sita wote wakiwa na ualbino.

“Niliona picha ya Jagadi mtandaoni,baada ya mmoja wa watu wenye mapenzi mema kuipost kuonesha jinsi ndugu yetu anavyopitia wakati mgumu baada ya kupata upofu wa macho,nimeamua kuja kumuona na tayari tumemjengea kibanda kwa ajili ya kufanyia biashara ya mkaa ambayo amekuwa akifanya ili kupata kipato kuendesha familia yake”,alieleza Mdimu.

“Nimetoka Dar es salaam kuja kumuona na kujionea hali halisi ya maisha yake,huyu ni baba mwenye mke na watoto sita,sasa haoni,tunaamini kibanda hiki kitamsaidia kuingiza kipato ili kuisaidia familia hii”,aliongeza Mdimu.

Alisema pia wamempatia magunia 18 ya mkaa kwa ajili ya biashara na kuahidi kuwasomesha watoto wawili kati ya 6 na kuahidi kutafuta kiwanja kwa ajili ya kuijengea nyumba familia hiyo ambayo inaishi kwenye nyumba ya kupanga.

Kwa upande wake,Jagadi aliishukuru taasisi ya Imetosha na Dar Marathon Club kwa msaada waliompatia na kubainisha kuwa banda hilo litamsaidia kupata pesa kwa ajili ya kuendeshea familia yake ambayo imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa chakula na kusababisha wakati mwingine kushinda na kulala na njaa.

“Nawashukuru sana kwa ufadhili wenu,kutoa ni moyo,natambua wapo watu wengi wana pesa na ninavyopata watu wa kunisaidia Napata faraja,Mungu awabariki sana”,alisema Jagadi.

Charles Kulwa Jagadi (41) amesema alianza kusumbuliwa na upele kwenye jicho lake la kushoto mwaka 2005,mwaka 2015 akaanza kupatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali ikiwemo KCMC,Bugando na Julai 22,2018 jicho lake liling’olewa katika hospitali ya taifa Muhimbili kwa kile alichoelezwa na Daktari kuwa ni Saratani ya Jicho.

Jicho lake jingine pia limepata upofu hivyo amejikuta hafanyi tena shughuli za uzalishaji mali kama ile kazi ya kuosha magari aliyokuwa anaifanya mwanzo ambayo ilikuwa inamsaidia kupata pesa kwa ajili ya kuendeshea familia yake.
Kulia ni Charles Kulwa Jagadi (41) mwenye Ualbino mkazi wa Kata ya Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga akimpokea Mtendaji Mkuu wa Imetosha Foundation,Henry Mdimu leo Jumapili Novemba 11,2018 kumtembelea.Nyuma ni kibanda cha biashara ya mkaa kilichojengwa kwa ufadhili wa Imetosha Foundation na Dar Marathon Club kwa ajili ya Charles Kulwa Jagadi - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mtendaji Mkuu wa Imetosha Foundation,Henry Mdimu (wa pili kulia) akijitambulisha kwa Charles Kulwa Jagadi (kulia).Wa kwanza kushoto ni mke wa Jagadi Esther Shija akifuatiwa na Mratibu wa Imetosha Foundation Kanda ya Ziwa,Janeth Chijanga.
Charles Kulwa Jagadi (kulia) akieleza magumu aliyopitia hadi sasa amepata upofu wa macho.
Mtendaji Mkuu wa Imetosha Foundation,Henry Mdimu akizungumza na familia ya Charles Kulwa Jagadi.
Mtendaji Mkuu wa Imetosha Foundation,Henry Mdimu akimpatia fedha Charles Kulwa Jagadi kwa ajili ya kununulia mkaa na kununua mahitaji mengine ya familia.
Charles Kulwa Jagadi (kushoto) akimshukuru Mtendaji Mkuu wa Imetosha Foundation,Henry Mdimu kwa kumtembelea na kumjengea kibanda kwa ajili ya biashara ya mkaa.
Mtendaji Mkuu wa Imetosha Foundation,Henry Mdimu akipokea maelezo kutoka kwa fundi Paschal Manumbu John kuhusu ya ujenzi wa kibanda cha kuuzia mkaa cha Charles Kulwa Jagadi.
Muonekano wa kibanda cha kuuzia mkaa cha Charles Kulwa Jagadi kilichojengwa kwa ufadhili wa Imetosha Foundation kwa kushirikiana na Dar Marathon Club.
Muonekano wa kibanda cha kuuzia mkaa cha Charles Kulwa Jagadi.
- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post