POLISI WAONESHA NYUMBA ALIYOHIFADHIWA MO DEWJI BAADA YA KUTEKWA


Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ameonyesha nyumba anayodaiwa kuhifadhiwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ baada ya kutekwa na watu ambao mpaka sasa hawajajulikana.


Mo Dewji (43), alitekwa Oktoba 11,2018 alfajiri katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam nchini Tanzania alikokwenda kufanya mazoezi lakini alipatikana Oktoba 20 katika viwanja vya Gymkhana baada ya kutelekezwa na watekaji.


Leo Jumapili Novemba 11, 2018 mbele ya wanahabari, Kamanda Mambosasa ameonyesha nyumba hiyo yenye ghorofa moja iliyopo Mtaa wa Mwansasu Mbezi Beach jinini hapa.


Amesema baada ya mfanyabiashara huyo kupatikana polisi waliendeleza msako na kufanikiwa kuipata nyumba hiyo iliyopo umbali kilomita moja toka barabara ya Old Bagamoyo.


"Nyumba hii ndipo alipokuwa akihifadhiwa Mo baada ya kutekwa, Nyumba hii ni ya marehemu Mwansasu lakini sasa hivi inamilikiwa na binti zake,” amesema Mambosasa.


"Katika nyumba hii walitokea watu waliojitambulisha kuwa ni wafanyabiashara wa madini kutoka Afrika Kusini walipanga lakini walipitia kwa Twalib Mussa," amesema.


Kamanda Mambosasa amesema makubaliano yaliyokuwapo ni wafanyabiashara hao kulipa Dola za Marekani 1,500 (Sh3.4 milioni) kwa mwezi huku wahusika wa nyumba wakipata dola 1,300 huku Mussa aliyefanikisha wafanyabiashara kupata nyumba hiyo akiambulia dola 200.


Kwa upande wake, Twalibu ambaye ni dereva wa teksi anayefanya shughuli zake Hotel ya Whitesands amesema yeye ndio aliyefanikisha wafanyabiashara hao kupata nyumba hiyo baada ya kuwaunganisha na madalali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527