Picha : PACESHI YAFUNGA MAFUNZO KWA WASAIDIZI WA KISHERIA KISHAPU NA SHINYANGA...HAKIMU ASEMA KUNA HOFU YA MAHAKAMA

Imeelezwa kuwa wananchi wengi hususani maeneo ya vijijini bado hawana uelewa wa sheria na kutawaliwa na hofu ya kwenda mahakamani kudai haki zao na kuishia kutumia pesa nyingi kumaliza kesi zao kimya kimya.

Hayo yamesemwa leo Novemba 22,2018 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ushetu Happiness Mtawala akimwakilisha Hakimu Mfawidhi Mwandamizi wa wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya Wasaidizi wa Kisheria na msaada wa kisheria yaliyoandaliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria Shinyanga (Paralegal Aid Center Shinyanga – PACESHI) kwa ufadhili wa Legal Services Facility (LSF).

Mafunzo hayo yaliyolenga yamefanyika katika ukumbi wa Nitesh mjini Kahama na kushirikisha wasaidizi wa kisheria kutoka halmashauri ya wilaya ya Kishapu,Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga ambao wamejengewa uwezo juu ya masuala ya kisheria ili wakaisaidie jamii.

Hakimu Mtawala alisema watu wengi wamekuwa wakiogopa kwenda mahakamani,wakidhani kuwa mtu akifika tu mahakamani basi anafungwa matokeo yake wamekuwa wakiishia kutoa pesa na kumaliza kesi hivyo kukosa haki zao.

Mtawala aliwataka wasaidizi hao wa kisheria kuongeza juhudi katika kuwasaidia wananchi kwani wengi hawajui sheria, wanadanganywa matokeo yake kesi zinaishia kwenye ofisi za serikali za mitaa hivyo wawaelekeze wakapate haki mahakamani.

"Naomba mkawaelimishe wananchi kwani wengi hawana mwamko wa kisheria,mahakama ipo kwa ajili yao waelekezeni wafike mahakamani ,mtu anaogopa mahakama utafikiri kitu gani sijui.....

Mahakama ni sehemu ya mtu kumpatia haki,siyo sehemu ya mtu kuwa na uoga kuwa ukifika pale unafungwa,ukifika pale pande zote zinasikilizwa,wewe huna hatia mpaka ithibitishwe kuwa una hatia, mahakama ndiyo sehemu pekee ambapo haki hutolewa sisi huwa tunaangalia sheria inasemaje kisha tunatoa uamuzi ",alisema Mtawala.

Kwa upande wake,Wakili wa Serikali Geofrey Kesase aliyemwakilisha Msajili wa watoa huduma ya msaada wa kisheria Wizara ya Katiba na Sheria, alisema wasaidizi hao wa kisheria sasa wanatambuliwa na kisheria hivyo kuwataka kuzingatia,sheria,kanuni na miongozo iliyowekwa ili kutekeleza vyema majukumu yao.

"Usitoke hapa ukajiita kuwa mimi sasa ni wakili, wakili ana sheria,kanuni na miongozo na mipaka yake,ukienda kinyume utakuwa unatenda kosa la jinai,naomba mtekeleze majukumu yenu,toeni msaada,shirikianeni katika kutoa huduma kwa wananchi”,alisema Kesase.

Naye Meneja Mradi wa Kuboresha Huduma za Msaada wa Sheria Kupitia Wasaidizi wa Kisheria wa PACESHI,John Shija alitumia fursa hiyo kulipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha sheria ya msaada wa kisheria.

Alisema suala la msaada wa kisheria lilikuwa ni kilio cha wananchi wengi hivyo serikali imekata kiu ya wananchi hususani,wanawake,watoto na wazee ambao wanahitaji sana msaada wa kisheria.

"Naishukuru serikali kwa kuandaa mswada wa sheria ya msaada wa sheria hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Magufuli kusaini na kupitisha sheria No.1/2017 ya msaada wa sheria, sasa kuna uhusiano wa karibu kabisa kati ya watoa huduma za kisheria na wahitaji wa msaada wa kisheria”,alieleza Shija.

Aidha aliishukuru Shule ya Sheria kwa vitendo "The Law school of Tanzania" kwa kuandaa mtaala maalum wa wasaidizi wa kisheria ambao unatumika kuwafundishia wasaidizi wa kisheria katika halmashauri mbalimbali nchini.

Alisema PACESHI ilitarajia kutoa mafunzo wasaidizi wa kisheria 110 kutoka halmashauri sita za mkoa wa Shinyanga ambazo ni Shinyanga,Manispaa ya Shinyanga,Kishapu,Kahama Mji,Msalala na Ushetu lakini imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria 109.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ushetu, Happiness Mtawala akifunga mafunzo ya siku tano ya Wasaidizi wa Kisheria na msaada wa kisheria yaliyoandaliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria Shinyanga (Paralegal Aid Center Shinyanga – PACESHI) kwa ufadhili wa Legal Services Facility (LSF) leo katika ukumbi wa Nitesh mjini Kahama - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ushetu, Happiness Mtawala akifunga mafunzo ya siku tano ya Wasaidizi wa Kisheria na msaada wa kisheria. Aliwasisitiza wasaidizi hao wa kisheria kuepuka kupokea pesa kutoka kwa raia wanaowapa msaada wa kisheria kwani kazi yao ni ya kujitolea.
Wasaidizi wa Kisheria na msaada wa kisheria wakimsikiliza Hakimu Mtawala.
Awali Wakili wa Serikali Geofrey Kesase aliyemwakilisha Msajili wa watoa huduma ya msaada wa kisheria Wizara ya Katiba na Sheria akijitambulisha kwa mgeni rasmi Hakimu Happiness Mtawala (kushoto) wakati wa kufunga mafunzo hayo.Kulia ni Mkurugenzi wa PACESHI,Perpetua Magoke.
Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Shinyanga (Paralegal Aid Center Shinyanga – PACESHI),Perpetua Magoke akizungumza wakati wa mafunzo ya siku tano ya Wasaidizi wa Kisheria na msaada wa kisheria kutoka halmashauri ya wilaya ya Kishapu,Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga.
Mkurugenzi wa PACESHI ,Perpetua Magoke akiwasitiza wasaidizi wa kisheria kuzingatia sheria,kanuni na miongozo wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kutoa huduma na msaada wa kisheria kwa wananchi.
Wakili wa Serikali Geofrey Kesase aliyemwakilisha Msajili wa watoa huduma ya msaada wa kisheria Wizara ya Katiba na Sheria akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Watoa huduma na wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini.
Meneja Mradi wa Kuboresha Huduma za Msaada wa Sheria Kupitia Wasaidizi wa Kisheria wa PACESHI,John Shija akizungumza wakati  wa kufunga mafunzo ya Wasaidizi wa Kisheria na msaada wa kisheria.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Meneja Mradi wa Kuboresha Huduma za Msaada wa Sheria Kupitia Wasaidizi wa Kisheria wa PACESHI John Shija alisema PACESHI imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria 109 katika halmashauri sita za mkoa wa Shinyanga ambapo matarajio ilikuwa kufikia wasaidizi wa kisheria 110.
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Mwenyekiti wakati wa mafunzo hayo,Zacharia Mkumbo akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo na kuahidi kuzingatia mambo yote waliyofundishwa kwenye mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa siku tano mjini Kahama.
Picha ya pamoja baada ya kufunga mafunzo hayo.
Picha ya pamoja.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Soma Pia : PACESHI YAENDESHA MAFUNZO KWA WASAIDIZI WA KISHERIA MSALALA,USHETU NA KAHAMA MJI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527