DC MAHUNDI AITAHADHARISHA KAMATI YA UJENZI WA KITUO CHA AFYA MTANDE CHUNYA

Serikali wilayani Chunya mkoa wa Mbeya, imeitahadharisha Kamati ya Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mtande kinachojengwa katika Kata ya Mmba wilayani humo kuepuka matumizi mabaya ya fedha za serikali.


Tahadhari hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya hiyo, Maryprisca Mahundi alipofanya ziara ya kukakua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambapo aliwataka kuhakikisha fedha zilizotolewa na serikali zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wa vijiji kata na tarafa wamekuwa na tabia ya kutengeneza mazingira ya ubadhirifu wa fedha za miradi ya wananchi hasa zile zinazokusanywa kutoka kwa wananchi wa maeneo husika.

Aliwataka waweke wazi matumizi ya fedha zote ili kuepuka sintofahamu ya fedha hizo zinazotolewa na serikali pamoja na michango ya wananchi na wakaonekana kama wapigaji kitu ambacho alisema kinaweza kikawaletea matatizo.

“Ni bora mkaweka wazi fedha mnazotakiwa kulipwa, ionekane msimamizi wa mradi alilipwa kiasi fulani  kuliko ije ibainike kuwa kuna fedha ‘inahang’ (inaning’inia) haieleweki ilitokaje, kwa sasa hivi tutakuwa wakali  na tutafuatilia sana,” alisema Mahundi.

Alisema Serikali haitasita kumchukulia hatua za kisheria kiongozi yeyote atakayebainika kuwa ni mbadhilifu wa fedha za miradi ya wananchi ili kuhakikisha kila mradi unatekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mamba, Ramadhani Shumbi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya alisema ujenzi wa kituo hichounaenda vizuri na kwa kasi inayotakiwa.

Alisema mradi huo unatekelezwa na wananchi wa Kata hiyo yenye vijiji vitatu pamoja na Serikali kuu kupitia Wizara ya Ofisi ya Rai Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na kusimamiwa na halmashauri ya wilaya hiyo.

Shumbi alisema Serikali kuu imetoa shilingi milioni 400 huku wananchi wakichangia zaidi ya shilingi milioni 50 ambazo ni fedha taslimu pamoja na nguvu yao ya kubeba mawe, mchanga na kokoto kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Alisema baadhi ya majengo yameshaezekwa kikiwemo chumba cha kuhifadhi maiti huku baadhi ya majengo zikiwemo wodi, chumba cha upasuaji pamoja na nyumba ya kuishi watumishi yakiwa yanaezekwa.

“Ujenzi wa kituo hiki cha mamba – mtande tuna mwezi mmoja na nusu toka tumeanza lakini tuna speed nzuri (mwendo) na lengo letu ni kuhakikisha kwamba tukichelewa sana basi tumalize mwezi januari lakini lengo letu hasa ni kumaliza mwezi disemba,” alisema Shumbi.

Baadhi ya wananchi wa Kata hiyo walisema kuwa walihamasika kuchangia ujenzi wa Kituo hicho kutokana na kuishi mbali na huduma ya afya na kwamba walikuwa wanategemea Hospitali ya Wilaya ambayo iko mbali.

Mmoja wa wananchi hao, Nesi Michael, alisema wanawake ndio wanaopata shida zaidi kutokana na kuwa mbali na huduma za afya kwa madai kuwa walikuwa wanapata shida wanapokuwa wanataka kujifungua.


Alisema hata barabara wanayoitumia kutoka katika kata hiyo mpaka hospitali ya Wilaya ni mbaya hivyo walikuwa wanafika hospitalini wakiwa na hali mbaya.

Na Davidi Nyembe, Chunya
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Maryprisca Mahundi akiwa katika kituo cha Afya cha Mtande kinachojengwa katika Kata ya Mmba 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post