SERIKALI YATOA BILIONI 21 UJENZI MIUNDOMBINU MTWARA


Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa (mwenye shati Jeupe) akikagua ujenzi wa mfereji wa maji kutoka Skoya, Nabwaba, Shakuru hadi Mtepwezi.
Mfereji wa kuondoa maji kutoka Skoya, Nabwada Shakuru hadi Mtepwezi
Ujenzi wa soko la Chuno

Na Evaristy Masuha - Mtwara 

Serikali kupitia mradi wa uendelezaji miji Mkakati (Tanzania Strategic Cities Project) imetoa bilioni 21.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimblai ya maendeleo katika Manispaa ya Mtwara mikindani. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara 4 za mitaa kwa kiwango cha lami, Ujenzi wa maeneo matatu ya kupumzikia (Recreation Center), mfereji mkubwa wa kuondoa maji ya mvua, ujenzi wa soko la kisasa pamoja na kituo cha daladala eneo la Mikindani.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa wilaya ya Mtwara Mhe. Evod Mmanda amesema fedha hizo zimetolewa kwa mkopo na Benki ya dunia na kwamba ujenzi wa miradi hiyo yote inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2019.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa  Gelasius Byakanwa amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutaufanya mji wa mtwara kuwa na muonekano mzuri na kwamba hiyo ndiyo hatua nzuri kuifanya Manispaa kuwa na sifa ya kuwa Jiji.

“Naamini baada ya kukamilika miradi hii Mtwara itakuwa sehemu nyingine na pengine inaweza kupata sifa ya kuelekea kuwa jiji”.

Amewataka vijana waliopata nafasi ya kuajiliwa katika ujenzi wa miundombinu hiyo kuwa waamifu ili kujijengea imani kwa waajiri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527