WEZESHA FOUNDATION YAANZA KUTOA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA VIJANA NA WANAWAKE KIGOMA


Na Rhoda Ezekiel Kigoma
 Kufuatia kauli mbiu ya serikali ya hapa kazi tu ,Taasisi isiyo ya Kiserikali  ya Wezesha Foundation  imeanza kutoa mafunzo kwa Vijana na Wanawake ya kutambua fursa zilizopo mkoani Kigoma na namna gani watazitumia kwa kufanya biashara na kukuza uchumi wa wananchi wa mkoa wa Kigoma.


Akizungumza jana wakati wa Uzinduzi wa Taasisi hiyo, Mkurungenzi wa Taasisi  Wezesha ambaye pia ni mbunge wa Vijana Taifa Zainabu Katimba, alisema taasisi hiyo imelenga  kuwafikia wanawake na vijana 800 kwa awamu ya Kwanza kwa kutoa mikopo na mafunzo ya ujasiriamali na kujifunza fursa zilizopo mkoani Kigoma ili waweze kuzitumia na kuhakikisha wanaiunga serikali mkono kwa kuanzisha viwanda na kuwawezesha Kuenda na kasi ya uchumi wa kati.

Alisema taasisi hiyo pia inajihusisha na kufanya shughuli mbali mbali za Kijamii kama kutembelea shule na kutatua kero za Wananchi, kuchangia maendeleo ya wananchi pamoja na kuisaidia jamii  na lengo kubwa la kufanya hivyo ni kuisaidia jamii ya wanakigoma na kuhakikisha Kigoma inaendana na kasi ya mikoa mingine.

"Siku hii ya leo tumeanza mafunzo ya ujasiriamali na mafunzo hayo yameanza kwa wilaya tatu, Kigoma Mjini , Kigoma Vijijini na Uvinza na  tumeshirikiana na watu wa Sido na Ofisa maendeleo pia tutaendelea kwa wilaya zingine zilizo baki lengo ni kuhakikisha tunawafikia vijana wote na wanawake wenye lengo la kufanya biashara na kujituma na walioshindwa namna gani ya kuanza biashara zao", alisema Zainabu.

Pia alisema wameamua kushirikiana na Serikali kwa kutoa mafunzo kwa Vijana na wanawake kutambua namna gani watakavyo unda vikundi na kuweza kunufaika na fedha za halmashauri  za asilimia 10% ya wanawake na Vijana ambazo zipo na hazitumiki kama ilivyopangwa na serikali.

Akizungumza na wanawake na Vijana wakati wa semina hiyo, Ofisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Kigoma Zilpa Kisonzela ,  alisema Wanawake na vijana wanatakiwa kuunda vikundi na  vikundi hivyo viwe na mipango mizuri na kila mikundi kinatakiwa kiwe na shughuli ambazo wanazifanya na mambo ambayo yanaonekana.

Alisema ili Halmashauri ziweze kutoa fedha katika makundi ya vijana na Wanawake ni lazima makundi hayo yawe na mtaji na shughili ambazo wanazifanya kwa ajili ya maendeleo na kujiongezea kipato na halmashauri zinatoa fedha kulingana na shughuli ambazo zinafanywa na kikundi na fedha ambazo wamekwisha tengeneza serikali inawawezesha.

Alisema vikundi vinavyopatiwa mikopo ni vikundi vya kijamii na sio vikundi vya ,chama, Kanisa au jumuiya flani ni vikundi ambavyo vimesajiliwa kisheria na vinatumiwa na jamii fulani na havina mfungamano na taasisi ya kidini wala chama.

Nao baadhi ya Wananchi wa Mkoa wa Kigoma Magreth  Bernard ni mmoja kati ya wanufaika wa taasisi hiyo alimpongeza mbunge huyo na kuendelea kuiomba Serikali fedha hizo zinazo pangwa kwajili ya makundi maalumu zitolewe, kwa kuwa vijana wengi na wanawake wanamalengo makubwa ya kufanya biashara na kuinua uchumi lakini wanakwama katika mtaji.

Alisema wengi wamekuwa wakienda kuomba mikopo katika halmashauri na wanazungusha na fedha hawapati, na fedha wanazopatiwa hazitoahi kuwagawia wanakikundi wote waweze kufanya biashara na kuzalisha kwa wingi, na endapo watapatiwa mikopo wanauhakikia wa kufanya vizuri katika shighuli za maendeleo.

Shabani Husein ni Kijana ambae ameziona fursa mkoani Kigoma na kuanza kuzitumia alisema Kigoma kuna fursa ya Kilimo, Uvuvi na shughuli zingine endapo vijana watawezeshwa wanauwezo wa kufanya mabadiliko makubwa na kuhakikisha mkoa huo unainuka kiuchumi kwa kuwa vijana ni nguvu kazi ya Taifa na wakiwezeshwa wanaweza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527