WAZIRI MBARAWA AKERWA NA WAKANDARASI WABABAISHAJI

Mhandisi wa Maji Wilaya ya Nanyamba, Moses Msuya akimuonyesha Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa mpango ya utekelezaji wa mradi wa Nanyamba-Mlanje.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akikagua matenki ya mradi wa Nanyamba-Mlanje katika Wilaya ya Nanyamba, mkoani Mtwara.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiwa kwenye mradi wa Mkwiti, katika wilaya Tandahimba, mkoani Mtwara.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Newala, akiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Aziza Mangosongo.
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akisikiliza taarifa inayosomwa na Mhandisi wa Maji Wilaya, Nsajigwa Sadiki. 


………………………….


Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amekerwa na wakandarasi wababaishaji ambao wamekuwa wakichangia miradi mingi ya maji kuchelewa kukamilika au kujenga miradi yenye viwango duni na kuisababishia Serikali matatizo na wananchi wake.

Hali hiyo imetokana na kukosekana kwa mkandarasi katika eneo la kazi kwenye mradi wa Nanyamba-Mlanje, katika Wilaya ya Nanyamba mkoani Mtwara wakati alipofika kukagua mradi, kitendo ambacho hakukifurahia.

Profesa Mbarawa amesema alitegemea kumkuta mkandarasi huyo site ili aweze kuzisikia changamoto zinazomkabili na kuzipatia ufumbuzi ili mradi huo uweze kukamilika mara moja na kutoa huduma.Akiongea na wakazi wa Mlanje, Profesa Mbarawa amesema ametoka kuidhinisha malipo ya Shilingi Milioni 93 kwa mkandarasi huyo wiki iliyopita lakini ameshangazwa na kutomkuta akifanya kazi, na kuwaambia wakandarasi wasiokaa site ni wababaishaji na hawafai.

“Wakandarasi wa namna hii ni wababaishaji hawatufai na siwataki kwa sababu wanaigombanisha Serikali na wananchi, wakikwamisha mipango ya Serikali na wananchi wakiendelea kukosa maji bila sababu za msingi. Sitaki wakandarasi wa aina hii na ndio maana tumewafukuza waliokuwa kwenye miradi ya Kigoma na Lindi kutokana na tabia za ubabaishaji’’, amesema Profesa Mbarawa.

“Ni lazima popote kwenye miradi ya maji nitakapotembelea nikute mkandarasi akiwa site, sitaki jambo hili lijirudie tena. Nataka wakandarasi wanaothamini kazi tunazowapa na kumaliza kwa wakati”, amesisitiza Profesa Mbarawa.

Akiwa katika Wilaya ya Tandahimba, Profesa Mbarawa ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya vijiji 10 wilayani humo, ambapo miradi ya vijiji 6 vya Likolombe, Kidoo, Malamba, Matogoro, Mihambwe na Mkupete imekamilika baadhi ya miradi hiyo ikiwa ni mipya na mingine imefanyiwa upanuzi.

Wakati miradi iliyobaki ya vijiji 4 vya Chaume-Mkonjowano ukarabati wake umekamilika, Mahuta ukarabati na upanuzi umekamilika, Jangwani-Maheha ukarabati wake umefikia asilimia 95 na Litehu-Libobe ukarabati na upanuzi wake umefikia asilimia 95.

Pia, Serikali inatekeleza mradi wa Mkwiti wilayani Tandahimba ambao utaongeza huduma ya maji kwa wananchi wapatao 21, 384 katika vijiji 14, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II) ambao kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 66 na utagharimu Shilingi Bilioni 8.5.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527