WAZIRI AGEUKA MBOGO WALIMU KUVUJISHA MITIHANI ...'SITARAJII KUSIKIA SUALA HILI TENA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya maafisa elimu na walimu kutojihusisha na vitendo vya wizi wa mitihani vinavyofanywa kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kwa sababu vinawadharirisha.

“Kama kweli umemuandaa mtoto huna sababu ya kuiba mitihani na mtoto hawezi kufikiria kuiba mitihani kwa sababu yuko nje ya mfumo. Walimu heshimuni maadili ya kazi ya ualimu.”

Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumanne, Oktoba 9, 2018) baada ya kukabidhiwa vyumba vya madarasa vya shule za msingi Nyakato na Kashozi, wilayani Bukoba.

Vyumba hivyo vilivyojengwa kwa msaada wa Serikali ya Japan baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera mwaka 2016.

Waziri Mkuu amesema tathmini ya elimu katika shule za msingi na sekondari hufanyika kwa kufanya mitihani, dosari ya udanganyifu wa mitihani iliyojitokeza katika mitihani ya darasa la saba mwaka huu isijirudie tena.

Wiki iliyopitaBaraza la Mitihani la Taifa (NECTA) lilifuta matokeo ya mitihani ya darasa la saba kwa shule za msingi zote za Halmashauri ya Chemba na baadhi ya shule katika halmashauri ya Kondoa, Kinondoni, Mwanza jiji na Ubungo kwa kosa la kuvujisha mitihani.

Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imechukua hatua kali kwa watu wote walioshiriki katika kitendo hicho kwa sababu kinadumaza uelewa na ufikiri kwa wanafunzi, hivyo kuwaandaa watoto kuwa wategemezi.

“Hata hivyo, Serikali inaendelea na uchunguzi juu ya suala hili ili kubaini chanzo cha wizi huo. Walimu, kitendo cha kumpa mtoto mitihani ni sawa na kujiaibisha kwani mnaonekana hamjafanya kazi zenu ipasavyo. Sitarajii kusikia suala hili tena.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametembelea kiwanda cha kahawa cha Amimza ambacho ni kati ya viwanda vikubwa vitano vya kusindika kahawa Barani Afrika, ambapo ametumia fursa hiyo kumpongeza mwekezaji mzawa Bw. Amiri Hamza na kumuhamasisha aongeze uzalishaji.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametembelea kituo cha utafiti Maruku ambapo alikagua na kupokea taarifa za shughuli za utafiti wa zao la kahawa na alitumia fursa hiyo kuwashauri wakulima wenye miti mikongwe kung’oa na kupanda mipya kwa awamu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post