Picha: TCRA YAKUTANA NA VIONGOZI SHINYANGA..YAWATAKA WAMILIKI WA VING'AMUZI NA VISIMBUZI KUHESHIMU SHERIA


Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) imesisitiza juu ya umuhimu wamiliki wa ving'amuzi na visimbuzi vinavyorusha matangazo yake hapa nchini kuheshimu sheria na kuhakikisha wana leseni zinazowaruhusu kuonesha chaneli za ndani bure badala ya kuwatoza wananchi fedha yoyote.

Hali hiyo imebainishwa leo Oktoba 3,2018 mjini Shinyanga kwenye semina ya siku moja iliyoendeshwa na Mamlaka hiyo kwa viongozi mbalimbali wa serikali, mashirika ya umma na asasi za kiraia mkoani Shinyanga.

Semina hiyo ililenga kuwapa uelewa viongozi hao juu ya sababu za TCRA kufungia baadhi ya ving’amuzi kurusha chaneli za ndani baada ya kubaini vimekiuka masharti ya leseni zao ambapo hata hivyo lengo ni kumwokoa mtumiaji wa ving’amuzi na visimbuzi kutotozwa gharama kubwa.

Mtoa mada katika semina hiyo, Mhandisi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Francis Mihayo alisema lengo la mamlaka hiyo ni zuri ambalo limezingatia sheria za mawasiliano nchini.

Mihayo alisema maamuzi yaliyochukuliwa na TCRA kuagiza kuondolewa kwa chaneli za ndani kwenye baadhi ya ving’amuzi na visimbuzi vya makampuni ya DSTV, AZAM TV na Zuku TV ambavyo havikuwa na leseni ya kurusha chaneli za ndani umelenga kusimamia sheria zilizopo.

Alisema ving’amuzi vilivyozuiliwa vinapaswa kuheshimu sheria za nchi na kwamba vituo vilivyoshinda tenda ya kuonesha chaneli za ndani zipatazo nane ndizo zinazopaswa kuonesha chaneli hizo na si vituo vingine.

Alifafanua kuwa baada ya kuhama kutoka kwenye analojia kuja digitali, serikali iliweka sheria na taratibu ambazo zinatakiwa kufuatwa ili jamii iendelee kunufaika na uhabarishwaji pasipo kurudishwa nyuma na gharama kubwa.

"Kuna kitu kinaitwa FTA (hii ni ya kurusha Maudhui Bila kulipia) na vipindi vya kutolipia ni Vipindi vya Kijamii ikiwemo taarifa ya Habari, vinapaswa kuwa Bure.

Na kuna mfumo wa (Subscription by payment) pay TV yaani watumiaji wanapata vipindi vya TV kwa kulipia, na hivi vipindi ni vile ambavyo si vipindi vya kijamii.

Lakini kumekuwa na kuchanganya mambo ambapo Ving'amuzi huwalipisha watu na kwenye vipindi vya kijamii ambavyo vilipaswa kuonyeshwa bure kwenye ving'amuzi vyote.

Pia vipindi vya kijamii vilipaswa kutoonueshwa kwenye madishi ya satellite ambazo ni zakulipiwa moja kwa mpja kwani ni kukiuka masharti ya leseni yao",alisema Mihayo.

Awali mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akifungua semina hiyo amewataka viongozi wote waliohudhuria sheria hiyo kufikisha kwa wananchi elimu watakayoipata ili waelewe na waache kuilalamikia mamlaka ya TCRA wakidai haitendi haki.

Alisema lengo kuu la serikali ni kuhakikisha masharti ya leseni waliyopewa wamiliki wa ving’amuzi na visimbuzi yanaheshimiwa na kwamba kuwatoza wananchi malipo kwa chaneli zinazopaswa kuoneshwa bure ni kosa la kisheria.

“Ni vyema tukawa wanafunzi bora ili tuweze kuelewa masuala mengi yanayohusu sekta hii, kwani sisi sote ni wadau wakubwa wa sekta hii, ama kwa taarifa zetu kutangazwa kupitia vituo vya utangazaji au sisi wenyewe tuna visimbuzi majumbani mwetu kwa ajili ya kufuatilia na kusikiliza taarifa mbalimbali,”

“Ndugu washiriki maelezo yaliyotolewa kwa watoa huduma wa ving’amuzi vya AZAM, DSTV na Zuku yameangalia maslahi mapana ya taifa ikiwa ni pamoja na kumlinda mtumiaji wa mwisho kwa siku za mbeleni,” alieleza Telack.

Pia alisema iwapo TCRA wasingechukua hatua waliyoichukua hivi sasa watoa huduma hawa wangelazimisha huduma hii kwenye majukwaa yao na kuanza kupandisha bei taratibu kama wanavyotaka na hatimae wananchi wangeshindwa kumudu tozo zinazotozwa kila mwezi.

Kwa upande wao washiriki wa semina hiyo walishukuru kwa kupatiwa elimu iliyotolewa ambapo hata hivyo walichangia hoja mbalimbali na kuiomba TCRA kusimamia kwa ukaribu zaidi sheria zake ili wananchi watendewa haki badala ya kuumizwa kwa gharama za ving’amuzi wanazotozwa kila mwezi ambapo wameomba ikiwezekana gharama za sasa zipunguzwe kidogo.

Na Suleiman Abeid - Malunde1 blog

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akifungua semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA kwa viongozi mbalimbali wa serikali, mashirika ya umma na asasi za kiraia mkoani Shinyanga kwa ajili ya kuwapa uelewa viongozi hao juu ya sababu za TCRA kufungia baadhi ya ving’amuzi kurusha chaneli za ndani baada ya kubaini vimekiuka masharti ya leseni zao.Picha zote na Suleiman Abeid -Malunde1 blog
Mhandisi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Francis Mihayo TCRA Makao Makuu jijini Dar es Salaam akitoa mada wakati wa semina ya siku moja iliyoendeshwa na Mamlaka hiyo kwa viongozi mbalimbali wa serikali, mashirika ya umma na asasi za kiraia mkoani Shinyanga kwa ajili ya kuwapa uelewa viongozi hao juu ya sababu za TCRA kufungia baadhi ya ving’amuzi kurusha chaneli za ndani baada ya kubaini vimekiuka masharti ya leseni zao. 
Kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack wakisikiliza mada ukumbini.
Wakuu wa wilaya mkoani Shinyanga wakiwa ukumbini.
Viongozi mbalimbali wakifuatilia mada ukumbini.
Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga wakiwa katika ukumbi wa mikutano ya ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga.

Muandaaji wa vipindi vya TCRA kwenye vyombo vya habari vya Maadili na kizazi kipya (MAKIKI),Terry Gbemuu maarufu Mama Terry akiwa ukumbini.Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Meshimiwa Zainab Telack akizungumza wakati wa semina hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527