NDEGE YAANGUKA NA KUUA WATU WOTE WALIOKUWEMO


Ndege ya kuwabeba abiria ya shirika la Lion Air aina ya Boeing 737 imeanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege mjini Jakarta, maafisa wa Indonesia wamesema.

Ndege hiyo safari nambari JT-610 iliyokuwa imewabeba abiria 188 ilikuwa safarini kutoka mji huo mkuu wa Indonesia kwenda Pangkal Pinang, jiji linalopatikana katika visiwa vya Bangka Belitung.

Iitoweka kutoka kwenye mitambo ya rada saa kadha baada ya kupaa, ilipokuwa inavuka bahari.

Katika kikao na wanahabari, maafisa wamesema ndege hiyo, ambayo ni ndege mpya aina ya Boeing 737 MAX 8, ilikuwa imewabeba abiria 178 watu wazima, watoto watatu, marubani wawili na wahudumu watano wa ndege.

Yusuf Latif, msemaji wa shirika la huduma za uokoaji na kuwatafuta manusura amewaambia wanahabari: "Imethibitishwa kwamba ndege hiyo imeanguka."

Afisa wa shirika hilo la ndege ameiambia BBC kwamba bado hawajui chanzo cha kuanguka kwa ndege hiyo.

Afisa mkuu mtendaji Edward Sirait ameambia shirika la habari la Reuters: "Hatuwezi kusema chochote kwa sasa. Tunajaribu kutafuta maelezo na data zaidi."

Vyombo vya habari Indonesia vimemnukuu afisa wa bandarini Tanjung Priok akisema kwamba maafisa wa boti la kusindikiza meli wameripoti kwamba wameviona vifusi vya ndege hiyo kwenye mai.

Suyadi, ambaye hutumia jina moja pekee kama raia wengi wa Indonesia, amesema vyombo vingine vya baharini vimefunga safari kuelekea eneo hilo.

Ndege hiyo safari namba JT-610 iliondoka Jakarta saa 06:20 saa za huko Jumatatu asubuhi (23:30 GMT Jumapili).

Baada ya kusafiri kwa muda mfupi, ilitarajiwa kutua Pangkal Pinang saa moja baadaye.

Ndege hiyo inadaiwa kuwa Boeing 737 MAX 8, muundo wa ndege ambao umetumiwa kuanzia 2016.

Tovuti ya kufuatilia safari za ndege ya Flightradar24 inasema ndege hiyo iliwasilishwa kwa Lion Air mwezi Agosti.

Mtaalamu wa masuala ya uchukuzi wa ndege Gerry Soejatman ameambia BBC kwamba ndege hiyo aina ya MAX 8 imekuwa ikikumbwa na hitilafu tangu ilipoanza kutumiwa, saidi katika kupaa kwa utaratibu ufaao.Ndege hii ya Lion Air ilipaa baharini Bali mwaka 2013, lakini abiria wote walinusurika

Indonesia, taifa kubwa la mkusanyiko wa visiwa, hutegemea sana uchukuzi wa ndege, lakini ina historia ya ajali nyingi za ndege.

Lion Air ni shirika la safari nafuu za ndege.

Mwaka 2013, ndege ya Lion Air safari nambari 904 ilianguka baharini Bali ikijaribu kutua uwanja wa ndege wa Ngurah Rai.

Abiria wote 108 waliokuwa kwenye ndege hiyo walinusurika.

Mwaka 2004, ndege nyingine ya Lion Air safari nambari 538 kutoka Jakarta ilianguka na kuvunjika vipande vipande ilipokuwa inatua mjini Solo na kuwaua watu 25.
Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527