WAKULIMA WA MKONGE KOROGWE WATAKA HATI MILIKI


Singa (brashi) zikiwa kwenye Kiwanda cha Mkonge Magoma, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, zikiwa zinasubiri kwa miezi mitatu sasa, muafaka wa mgawanyo wa mapato kati ya wakulima na Katani Ltd, kabla ya kufungwa robota na kusafirishwa sokoni nje ya nchi. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkonge ukiwa umevunwa na kupangwa kwenye meta moja. Meta moja ina mizigo 110, na kila mzigo mmoja ni majani 30.

***
Na Yusuph Mussa, Korogwe

BAADHI ya wakulima Shamba la Mkonge Magoma, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamesema kama Serikali inataka kuwasaidia ili waweze kupata tija, basi jambo la kwanza ni kuwawezesha kupata Hati Miliki ya mashamba yao wanayolima mkonge.

Mashamba hayo ambayo wanayamiliki tangu kuanza kwa mfumo wa Wakulima wa Mkonge (SISO) ulioasisiwa na Kampuni ya Katani Ltd mwaka 1998, wakulima hao hawajapata hati, jambo linalowafanya wakose mikopo kwenye taasisi za fedha.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Oktoba 24 kwa nyakati tofauti, wakulima hao walisema kilimo cha mkonge kina manufaa makubwa, lakini ili kuyapata ni lazima uwe umewekeza kwa mtaji mkubwa, huku ukianza kuvuna baada ya miaka mitatu tangu kupanda zao hilo.

"Tunajua Serikali imeingilia kati kuona wakulima tunanufaika na mkonge. Pamoja na changamoto nyingine zilizopo kwenye kilimo hicho, lakini kubwa ni Hati Miliki ya kila mkulima mmoja mmoja anaemiliki shamba lake, apewe hati ili iweze kumsaidia kukopa kwenye taasisi za fedha za Serikali na zile za binafsi.


"Tangu kuanza kwa mfumo wa SISO, tuishukuru Kampuni ya Katani Ltd, kwani pamoja na kuasisi mfumo huu wa SISO, bado ilitusaidia kupata mikopo kwenye taaaisi za fedha pamoja na mifuko ya hifadhi kama NSSF, lakini huko tunakokwenda kama Serikali inataka tujitegemee bila kupitia mgongo wa Katani Ltd, basi ituandalie mazingira mazuri ya kujitegemea" alisema Abdi Shekighenda ambaye ni Mwenyekiti wa Wakulima (AMCOS) Shamba la Magoma.

Shekighenda ambaye ni mkulima wa mkonge tangu mwaka 2001 huku akiwa na hekta 32, alisema kilimo cha mkonge kutoka kuwa cha wawekezaji wakubwa wa kigeni na kuwa cha wakulima wadogo wa mkonge, kimeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wenyeji wanaoishi pembezoni mwa mashamba hayo ya mkonge.

"Tofauti na mazao mengine ambapo unaweza kulima, lakini wakati mazao yanakaribia kuivaa jua likawaka yakanyauka, na mfano halisi ni mahindi au maharage. Lakini kwa mkonge, limekuwa ni zao lisilotegemea mvua ama jua, kikubwa ni utunzaji tu. Wakulima wengi wa mkonge sasa hivi tumejenga nyumba, kununia magari na pikipiki.

"Hata wakati huu tukisubiri muafaka wa kugawanya maslahi sawa kati ya wakulima na Kampuni ya Katani Ltd, tuwaombe Serikali kuharakisha kumaliza suala hilo ili viwanda vya mkonge viifunguliwe na uzalishaji uendelee, kwani kuna matatizo mengi yanawakabili wakulima ikiwa ni pamoja na kupeleka watoto wao shule, chakula na mavazi" alisema Shekighenda.

Mkulima Ramadhan Kijangwa alisema mfumo wa SISO ukitimiza miaka 20, wakulima wamepata faida nyingi ikiwemo kuendesha maisha yao. Pamoja na changamoto zilizopo kwenye mfumo wa SISO, lakini anaamini mambo yatakaa sawa.

"Anachofanya Mkuu wa Mkoa wa Tanga (Martin Shigela), ambaye pia alikuja hapa kwenye shamba letu kutusikiliza, yupo sahihi kwa vile anapigania maslahi yetu. Ombi letu hili jambo la kutafuta kuweka maslahi ya wakulima kujua nani apate asilimia ngapi lisichukue muda mrefu.

"Kwani tangu Kiwanda cha Mkonge Magoma kimefungwa sasa unakwenda mwezi wa tatu, tunapata shida sana. Watoto wanapata mahitaji kwa tabu na mahitaji mengine. Lakini ikumbukwe wengine mkonge wao umekomaa, hivyo usipovunwa na kusindikwa, utaharibika.

Katibu wa AMCOS Shamba la Magoma ambaye pia ni mfanyabiadhara Athuman Kaoneka alisema biashara zao za maduka ya vyakula imeathirika kwa vile walikuwa wanategemea wafanyakazi wa kiwanda hicho na wakulima wanaouza mkonge wao, hivyo mzunguko wa pesa haupo tena.

Mfanyakazi wa Kiwanda cha Mkonge Magoma Nurdin Kauzeni alisema yeye ni mgonjwa wa saratani ya koo. Ili apate matibabu na gharama nyingine Hospitali ya Ocean Road, anatakiwa sh. milioni 1.8, na fedha hizo huwa anapewa na Katani Ltd, hivyo kwa kufungwa kiwanda hicho ameathirika kwa kiasi kikubwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post