SERIKALI YATOA ONYO KWA WATENDAJI WANAOTOA VITISHO KWA WALIMU


Katibu, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutaindurwa akitoa hotuba mbele ya Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule, Maafisa Elimu Kata na Wathibiti Ubora (hawapo pichani) wa Manispaa ya Jiji la Dodoma katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Dodoma. Kulia ni Kaimu Katibu Msaidizi Wilaya ya Dodoma, Bibi Leticia Mwakasitu na Kushoto ni Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Bw. Abdallah Membe.

***

Katibu, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu, Winifrida Rutaindurwa amewashauri watendaji wanaojikita katika kutoa vitisho kwa walimu badala ya kutafuta mbinu bora za kuwasaidia kuacha kufanya hivyo ili Walimu wasijiingize katika makosa ya kinidhamu kwa kisingizio cha kuogopa vitisho.

Rutaindurwa ametoa kauli hiyo hivi karibuni jijini Dodoma alipokutana na Maafisa Elimu, Wathibiti Ubora, Waratibu Elimu Kata (Maafisa Elimu Kata), Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Lengo la mkutano huo lilikuwa kuwaelimisha Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kuzingatia maadili na nidhamu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu pamoja na Miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali.

Alisema kuwa walimu hawapaswi kuishi kwa hofu kila wakati kutokana na vitisho wanavyopata kutoa kwa baadhi ya watendaji badala yake wanatakiwa kutekeleza majukumu yote kwa kuzingatia misingi na taratibu za utumishi wao.

Rutaindurwa alionesha kukerwa na baadhi ya watendaji wanaowasimamia walimu ambao kazi yao ni kutoa vitisho vya kuwafukuza kazi au kuwavua madakara endapo malengo flani hayatafikiwa bila kusaidia kutatua changamoto zinazokabili Walimu kufikia malengo.

“Unakuta mtu anakuambia wanafunzi wote wasipofaulu nakushusha cheo au nakufukuza lakini wala hamsaidii mkuu wa shule au mwalimu mkuu kutatua baadhi ya changamoto ambazo zipo ndani ya uwezo wake” alisema.

Aliongeza kuwa vitisho hivyo vimesababisha baadhi ya walimu kujikuta wakitenda makosa ya kinidhamu ili waonekane wamekidhi matakwa ya wanaowasimamia na matokeo yake wanachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.

“Sasa walimu lazima mtumie akili na sio kufanya vitu ili umridhishe mtu wakati unajiingiza katika hatari. Ukienda kuiba mtihani na kuwapa majibu wanafunzi ili ionekane shule yako imefanya vizuri hautabaki salama” alisema.

Aliongeza kuwa, “napenda muelewe kuwa ukitenda kosa usifikirie utakuja kujitetea kwa kusema nilifanya kwa vile niliambiwa nikaogopa, sisi tunakushughulikia wewe uliyekiuka maadili na taratibu za ualimu, unawajibika mwenyewe.”

Amesisitiza kuwa ni lazima mwalimu atekeleze wajibu wake kikamifu katika kufundisha ili wanafunzi wafaulu lakini baadhi ya watendaji nao hawapaswi kutoa vitisho vinavyomfanya mwalimu ashawishike kutenda makosa ili tu afikie malengo.

“Nimefurahi kwa kuwa Maafisa Elimu na Wathibiti Ubora mpo hapa. Nipende kuwasihi msiwatishe walimu kupita kiasi, wengine wanawatishia kuwafukuza kazi wakati mamlaka hayo hawana. Tuwahimize walimu kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia taratibu zinazotakiwa lakini tusipende kuwatwisha mizigo isiyoendana na uhalisia.

Aliongeza kuwa suala la kukuza elimu sio jukumu la mwalimu peke yake bali jamii wakiwemo viongozi, wazazi na walezi katika maeneo yao wana sehemu kubwa kusaidia kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha wanafunzi kufaulu.

“Wapo baadhi ya wazazi ambao hawafuatilii maendeleo ya watoto wao kabisa, wapo wengine ambao bado wanawafundisha watoto kuandika majibu ya uongo ili wasifaulu. Sasa hapa ni lazima viongozi kama madiwani na wengine wajitahidi kuwaelimisha wazazi ili waunge mkono juhudi za kuinua kiwango cha elimu”, alisema.

Alihitimisha kuwa Tume ya Utumishi wa Walimu ina wajibu wa kuwaelimisha walimu ili wasijihusishe na makosa ya kinidhamu katika utumishi wao na sio kwamba kazi kubwa ya Taasisi hiyo ni kusubiri walimu watende makosa ili iwafukuze kazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527