MIILI YA WATOTO WATATU YAKUTWA KATIKA GARI BOVU

Watoto  watatu wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia ndani ya  gari bovu la Toyota Mark X.

Walitoweka tangu Oktoba 15, mwaka huu  katika Mtaa wa Njaro wilayani Temeke,  Dar es Salaam.

Miili ya watoto hao, Jamila Mohamed (9), Amina Kunambi (7) na Yusuph Selemani (2) ilipatikana jana saa 4.00 asubuhi,   ndani ya gari hiyo iliyokuwa imeegeshwa kwenye gereji ya Inshallah inayomilikiwa na raia   mwenye asili ya Asia.

Miili hiyo ilipatikana  baada ya babu yao anayefanya kazi katika gereji hiyo kuhisi harufu ya mzoga hali iliyomlazimu kufanya upekuzi.

Taarifa za tukio hilo zilianza kusambaa katika mitandao ya jamii jana asubuhi ikieleza kuwa watoto hao wa familia moja walionekana wakiwa wamefariki dunia baada ya kupotea kwa siku tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari, baba mdogo wa watoto wawili kati ya watoto hao, Kagoda Issa, alisema tukio hilo ni la kutatanisha kutokana na mazingira ya watoto hao kupotea na kupatikana kwao kughubikwa na utata.

Issa alihoji watoto hao waliwezaje kuingia katika gari hilo na kujifungia mlango kiasi cha kushindwa kutoka wakati gari hilo limeharibika kwa muda mrefu.

“Tunashindwa kuelewa waliingia vipi wakajifungia wakati hata mfumo wa milango ya gari umekufa na baadhi ya vifaa vimetolewa.

“Tunashindwa kujua kama ni kweli waliingia kucheza wenyewe au ni mtu kafanya mambo yake halafu kawatupia humu,” alisema Kagoda.

Baba mzazi wa Amina, aliyekuwa akiishi na watoto hao, Omary Thomas, alisema   watoto hao waliondoka nyumbani kwao Mtaa wa Njaro Wilaya ya Temeke saa 10:00 jioni Oktoba 15, mwaka huu kwenda kucheza.

Alisema watoto hao  hawakurejea nyumbani hadi miili yao ilipokutwa kwenye gari hilo jana asubuhi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alidai kuwa watoto hao walikwenda lindoni kwa babu yao ambako waliingia ndani ya gari na kujifungia hivyo wakashindwa kutoka baada ya milango kujifunga.

“Nikiri kupokea taarifa ya vifo vya watoto watatu wa familia moja.

“Siku ya Jumatatu mama yake na mmoja wa watoto waliofariki dunia yaani mama yake Amina Kimambi, alifika na kutoa taarifa polisi, tulipokea hiyo taarifa na tukawashauri warudi wajiridhishe ili baada ya saa 24 waje waandikshe maelezo.

“Kwa hiyo ufuatiliaji wa tukio hilo ulianza na leo saa tano kasoro tulipokea taarifa kuwa mlinzi wa ile gereji alipokuwa akikagua lindo lake alipofungua mlango wa moja ya gari lilizokuwa katika gereji hiyo alithibitisha kuwapo miili ya watoto hao,” alisema Mambosasa.

Kamanda alisema jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo kubaini kama ni kweli watoto hao walifariki dunia baada ya kujifungia katika gari hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post