Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Isaya Mungure amesema mbunge wa chama hicho Arusha Mjini, Godbless Lema ameitwa polisi kufafanua kauli zake kuhusu tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’.
Mungure ambaye alikuwepo katika mahojiano ya awali kati ya Lema na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'azi amesema mbunge huyo ametakiwa kueleza ni kwa nini alitoa kauli kutaka wapelelezi wa nje ya nchi kuchunguza kutekwa kwa mfanyabiashara huyo.
Kwa upande wake, Lema amesema mara baada ya kufika hapo jeshi hilo lilimuhoji kuhusiana na masuala ya kutekwa kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji.
Kwa mujibu wa Godbless Lema ametoa maelezo kwa jeshi hilo ambapo amesema alishauri kuongeza nguvu juu ya namna ya kupambana na matukio ya kiuhalifu.
“Nimeandika kile ambacho nakijua na ni kile nilichokizungumza kwenye press, nimesema sitoacha kulikemea jeshi hilo na kulionya pale nitakapoona panafaa kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani.
"Kuna mashaka ambayo wanayo watu wengi kuhusu yaliyojitokeza kwenye hili suala, huwezi kuondoa mashaka hayo kwa kutisha watu bali kwa kuleta majibu, hivyo wasiyapuuze.
“Nipo tayari popote na kwa yeyote ku-defend kile nilichokisema kuhusu utekaji. Wakisoma wataona hiyo wanayosema kuisaidia polisi na nimewasaidia kwelikweli, hivyo.
“Wasione watu tunazungumza wakadhani kwamba tutatumiwa na mabeberu, hatutumiki Ila tunatafakari miaka 50 inayokuja jeshi la polisi litakuaje”.amesema Lema.
Akizungumzia kuhusu Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuzuia wananchi wasifanye mijadala ya tukio la utekani, Lema amesema waziri huyo hawezi kuzuia wananchi kuzungumza.
“Nimemwambia RPC wakinihitaji hakuna haja ya kufanya sinema za zamani za kuruka ukuta na kukata fensi, wanipigie tu nitakwenda mwenyewe kwa nauli yangu wala sitatumia mafuta yao,” alimaliza lema.