SERIKALI YATOA BIL 1.5 UJENZI HOSPITALI YA WILAYA YA BAHI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa tatu kulia) akipewa maelezo na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Bahi Dkt. Kassim Kolowa (kushoto) kwenye chumba cha upasuaji. 
****
Na Yusuph Mussa - Malunde1 blog Bahi

Serikali imetoa fedha sh. bilioni 1.5 ili kujenga Hospitali ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ikiwa ni mkakati wake wa kuboresha huduma za afya nchini.

Pamoja na fedha hizo, pia Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 kwa wilaya hiyo kwa ajili ya vituo vya afya vitatu vya Bahi, Mundemu na Chifutuka, ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi.

Hayo yalisemwa Oktoba 19, 2018 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye mkutano wa hadhara mjini Bahi mara baada ya kutembelea miradi mitatu ya nyumba ya kuishi walimu sita (Six in One), kufungua Daraja la Chipanga na ujenzi wa upanuzi wa majengo Kituo cha Afya Bahi.

Majaliwa alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani, imekuwa inapambana kuhakikisha huduma za jamii zinaboreshwa, na hilo wamefanikiwa, kwani wameweza kuongeza majengo kwenye vituo vya afya ili kuona wananchi wanapata huduma za afya za uhakika.

"Rais wetu Dkt. John Magufuli tangu Serikali yake imeingia madarakani amekuwa anapigania kuboresha huduma za jamii. Haya mapambano ya maendelei ni ya miaka yote, lakini yeye tangu ameingia anayafanya zaidi.

"Serikali imetoa sh. milioni 141 ili kujenga nyumba ya kuishi walimu sita kwenye Shule ya Sekondari Mpalanga, hatua ilipofikia ni nzuri, na fedha zimetumika vizuri, hivyo tutaongeza fedha ili kuukamilisha mradi huo. Pia tumejenga Daraja la Chipanga kwa sh. bilioni 2.1 na kutoa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya upanuzi wa majengo ya vituo vya afya vya Bahi, Mundemu na Chifutuka. Lakini kama haitoshi, tumetoa sh. bilioni 1.5 ili kujenga Hospitali ya Wilaya ya Bahi" ,alisema Majaliwa.

Alisema hata kwa huduma ya maji, wamepiga hatua kubwa, nia ikiwa kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akisalimiana na baadhi ya wagonjwa waliofika Kituo cha Afya Bahi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akifurahi jambo na mmoja wa akina mama aliyejifungua kwenye Kituo cha Afya Bahi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527