GARI LA TANROADS LATEKETEA KWA MOTO NA KUUA WATU WATATU,KUJERUHI SITA KAGERA


Watu watatu ambao majina yao hayajatambuliwa wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya gari linalomilikiwa na wakala wa barabara nchini (Tanroads) kugongana na gari jingine na kusababisha gari hilo kuwaka moto katika kijiji cha Mushasha wilayani Missenyi mkoani Kagera.


Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa wilaya ya Missenyi Kanali Denice Mwila alisema kuwa tukio lilitokea Oktoba 23 saa nane mchana, kwa kuyahusisha magari mawili likiwamo lenye namba za usajili STL 4842 linalomilikiwa na Tanroads likiendeshwa na dereva aitwaye Greyson Sospeter (40).

Kanali Mwila alisema gari hilo la Tanroads lilikuwa likitokea Ngara kuelekea Bukoba na kuwa liligongwa na gari la mizigo lenye chesis namba 500857 lilokuwa litokea jijini Dar-es-salaam kuelekea jamhuri ya Kidemokrasia Kongo likiendeshwa na Shebilal Patrice(38) raia wa Kongo.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari la mizigo kukwepa moshi mkuBwa bila kuchukua tahadhali kutokana na eneo la ajali kuwa na moto uliokuwa ukiwaka, na kuligonga gari hilo la Tanroads na kusababisha liangukie kwenye moto.

“Gari la Tanroads lilikuwa na abiria wanane na dereva akiwa wa tisa, walikuwemo wanawake watano na wanaume wanne, kwa bahati mbaya gari lilipowaka moto wanaume watatu waliungua moto na kufariki dunia” alisema.

Alisema kuwa dereva wa gari la mizigo anashikiliwa na polisi kufuatia tukio hilo na kuwa gari la Tanroads limeteketea kabisa na haliwezi kutengenezeka tena.

Kanali Mwila alisema kuwa miili yote ya marehemu na majeruhi imepelekwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kagera, isipokuwa dereva wa gari la Tanroads ambaye amepelekwa hospitali ya Omukajunguti, na kuwa majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu.

“Waliohusika katika ajali hiyo wengi ni vibarua wa Tanroads na hatujapata majina yao tunaendelea kufanya ufuatiliaji yatatolewa baadae” alisema kanali Mwila.

Alisema jeshi la zimamoto walifika na kuanza kuzima moto uliosababisha ajali hilo na kuwa magari yameruhusiwa kuanza kupita.

Akizungumza kwa njia ya simu kaimu kamanda wa polisi mkoani Kagera Issack Msengi alisema kuwa wapo kwenye kikao na kuwa atatoa ufafanuzi kuhusiana na tukio hilo baadae. 
Na Mwandishi wa Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527