JENESIA RUKYAA KUCHEZESHA MECHI YA SIMBA Vs YANGA SEPTEMBA 30


Jenisia Rukyaa ndiye refa atakayechezesha mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga Jumapili wiki hii Uwanja wa Taifa uliopo jijini Dar es Salaam akisaidiwa na Ferdinand Chacha na Mohamed mkono pembezoni mwa Uwanja na Mezani atakuwepo Elly Sasii.

Jenesia Rukyaa, refa wa Kagera tayari ana uzoefu wa kuchezesha katika michezo ya watani wa jadi kwa kuwa alishawahi kuchezesha mechi mbili.

Desemba 13, mwaka 2014 mechi ya Mtani Jembe, Simba SC wakishinda 2-0, mabao ya Awadh Juma na Elias Maguri na wa pili Februari 20, mwaka 2016 Yanga SC wakishinda 2-0, mabao ya Donald Ngoma na Amissi Tambwe.

Nyasi za uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam zitawaka moto Jumapili Saa 10:00 kwa mtanange wa watani wa jadi, Simba na Yanga.

Huo utakuwa mchezo wa pili kuzikutanisha timu hizo mwaka huu, baada ya Aprili 29 Simba SC kushinda 1-0, bao pekee la Erasto Edward Nyoni dakika ya 37, mechi ya marudiano ya msimu uliopita wa Ligi Kuu. 

Mechi ya kwanza ya msimu huo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 Oktoba 28 Uwanja wa Taifa Simba wakitangulia kwa bao la Shiza Kichuya dakika ya 57, kabla ya Obrey Chirwa kuisawazishia Yanga dakika ya 60. 

Simba SC wanatarajiwa kuingia kambini leo katika hoteli ya Sea Scape, Kunduchi jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Jumapili dhidi ya mahasimu, Yanga SC.

Uongozi wa Simba SC chini ya Rais wake, Salum Abdallah ‘Try Again’ ulipenda sana kuipeleka timu Zanzibar kama ilivyo kawaida, lakini kocha Mbelgiji Patrick J. Aussems amekataa hilo akisema ni kuwasumbua wachezaji.

Baada ya mapumziko ya siku moja timu ikirejea kutoka Kanda ya Ziwa kwa mechi nyingine za Ligi Kuu, SImba SC inatarajiwa kuendelea na mazoezi leo Uwanja wa Boko Veterani, nje kidogo ya mji.

Yanga SC waliondoka juzi kwenda mjini Morogoro kuweka kambi kujiandaa na mchezo huo, ikiwa ni siku moja tu baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Singida United kwenye mchezo mwingine wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa.

Huo ulikuwa ushindi wa nne mfululizo katika mechi zote nne za mwazo za Ligi Kuu, baada ya awali kushinda 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, 4-3 dhidi ya Stand United na 1-0 dhidi ya Coastal Union, zote Uwanja wa Taifa. 

Simba SC wataingia kwenye mchezo huo wakitoka kucheza mechi tano, wameshinda tatu 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, 2-0 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Taifa na 3-1 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, sare moja 0-0 na Ndanda FC mjini Mtwara na kufungwa moja, 1-0 na Mbao FC huko Mwanza.

Na Magdalena Kashindye - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post