RAIS MAGUFULI: KAMA MNAONA HII SHERIA HAIFAI NENDENI BUNGENI MKAIFUTE ILI WATU WAVUE TU SAMAKI WATAKAVYO


Rais Dkt. John Magufuli ameonyesha kukerwa na uvuvi haramu na kuwataka wanasiasa nchini kuliangalia kwa upana suala hilo na kama wanao halina tija kwa upande wao, amewaomba waende Bungeni wakaifute sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2005.


Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo jana akiwa wilayani Busega mkoani Simiyu katika muendeleo wa ziara yake ya kikazi aliyoanza Septemba 03, 2018 na kusisitizia kuwa anahitaji kuiona nchi ikizingatia sheria ambazo zimetungwa na watanzania wenyewe.

"Kama mnaona wanasiasa hili suala la mifugo na samaki halifai muende mkaifute hiyo sheria namba 22 ya mwaka 2005 ili watu wavue tu halafu muone baada ya miaka miwili kama mtakuwa na samaki hapa Busega. Ni lazima tuweke utaratibu na utaratibu ndio utakao ujenga hii nchi katika hali ya uchumi", alisema Rais Magufuli na kuongeza;

"Uvuvi haramu ni ugonjwa, siku za nyuma tulikuwa na samaki wengi sana hapa Busega lakini leo wote hawapo, mjue tumewamaliza sisi wenyewe. Madhara ya kuwamaliza samaki tumeyafanya sisi wenyewe"

Aidha, Dkt. Magufuli amewahakikishia wananchi wa Busega pamoja na watanzania kiujumla kuwa zoezi la kupambana na uvuvi haramu halitoweza kuisha kwa haraka kama baadhi yao wanavyofikiria na kuwataka wafahamu kuwa zoezi hilo ni endelevu.

"Nilipokuwa Waziri nilienda Magu na kuchoma nyavu sasa nimemuachia hii kazi Waziri Luhaga Mpina msimchukie anafanya kazi ya serikali, kwa niaba ya serikali kwa mujibu wa sheria ya namba 22 ya mwaka 2005. Na niwaombe ndugu zangu msinunue wala kuvua samaki wachanga", alisisitiza Rais Magufuli.


Mbali na hilo, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kuwachukulia hatua stahiki maofisa uvuvi endapo atabaini uvuvi haramu katika eneo analosimamia.

"Maofisa Uvuvi hawa ndio walioendeleza uvuvi huu haramu, na mimi nikuombe Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina anza kuwashughulikia maofisa uvuvi wako. Ukikuta mahali kuna uvuvi haramu na kuna ofisa uvuvi shika huyo muweke ndani, kwasababu wanalipwa pesa za serikali na uvuvi haramu unaendelea kwao",alisema Dkt. Magufuli.

Kabla ya agizo hilo la Rais Magufuli, itakumbukwa mnamo mwezi Februari mwaka 2018, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina alianzisha operesheni yake ya siku 40 katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa lengo la kupinga uvuvi haramu, ambao unakosesha fedha serikali kwa namna moja ama nyingine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post