POLISI DAR KUFANYIWA SHEREHE KWA KULINDA AMANI WAKATI WA UCHAGUZI UKONGA

Baada ya kumalizika kwa Uchaguzi wa ubunge Jimbo la Ukonga na Mwita Waitara wa CCM kuibuka mshindi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amemuagiza Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa kuitisha sherehe ya familia itakayowakutanisha askari -maarufu kama polisi family day.

Akizungumza jijini Dar es salaam Mkuu wa Mkoa Paul Makonda amempongeza Kamanda Lazaro Mambosasa kwa kusimamia zoezi la uchaguzi wa Ukonga na maeneo mengine ndani ya jiji hilo kwa kufanyika kwa amani.

“Kamanda Mambosasa andaa polisi family day nataka iwe siku ya mfano Tanzania, ili tupunguze msongo wa kazi ngumu mliyokua nayo wakati wa kulinda amani ya Dar es salaam…”

Aidha Paul Makonda amesema askari wa jeshi hilo watarajie kupata unafuu wa gharama za ujenzi kufuatia kiongozi huyo kuzungumza na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya saruji pamoja na kiwanda cha Mabati ili kuangalia namna ya kuliinua jeshi hilo.

Mapema leo katika ukumbi wa Anatoglo jijini Dar es salaam Msimamzi wa Uchaguzi ilala Jumanne Shauri alimtangaza Mwita Waitara wa Chama cha Mapinduzi kuwa mbunge mteule wa Ukonga kwa kupata jumla ya kura 77, 795 huku mpinzani wake CHADEMA Asia Msangi akipata kura 8676.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527