GEITA YAKUTANISHA MAKAMPUNI 250 KWENYE MAONYESHO YA DHAHABU


Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Maonyesho ya kimataifa ya teknolojia ya kisasa ya Uchenjuaji wa Dhahabu yanayofanyika katika uwanja wa CCM Kalangalala Wilaya na Mkoa wa GeitaMhandisi Chacha Wambura -Picha na Mutta Robert - Geita.
 ****
Maonyesho ya kimataifa ya teknolojia ya kisasa ya Uchenjuaji wa Dhahabu yanayofanyika katika uwanja wa CCM Kalangalala Wilaya na Mkoa wa Geita yanatarajiwa kuzikutanisha kampuni mbalimbali zaidi ya 250 na hadi sasa kampuni zaidi ya 150 zimeisha chukua mabanda na kuanza kuonyesha kazi zao.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maonyesho hayo Mhandisi Chacha Wambura amesema kuwa maonesho hayo yanatarajiwa kuwa na mabanda 250 ambayo yanajumuisha makampuni makubwa ya wachimbaji wa dhahabu,wachimbaji wadogo na kati pamoja na sekta mbalimbali zinazo unganishwa katika mnyororo wa thamani wa Dhahabu.

Kwa mujibu wa Chacha maonesho hayo yatafunguliwa rasmi tarehe 26 Septemba mwaka huu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na yatafika kilele chake tareh 30 Septemba mwaka huu.

Amesema maonesho hayo yatachochea ukuaji wa uchumi wa viwanda katika mkoa wa Geita na taifa kwa ujumla na kubadilisha mtazamo wa walio wengi kuhusu kutumia teknolojia ya kisasa katika utafutaji,uchimbaji na uchemjuaji wa kisasa ili kuondokana na dhana potofu na matumizi ya teknolojia hafifu.

Naibu Kamishna wa Wizara ya Madini Joseph Ngurumo amesema wanatumia maonyesho hayo kuelimisha jamii kuhusu jinsi gani ya kutafiti dhahabu,kuchimba,kutumia tafiti za kijiolojia na kuwaelimisha wachimbaji wadogo wadogo namna ya kupata mikopo.

Naye Afisa Mwajiri wa kampuni ya serikali ya uchimbaji wa Dhahabu (STAMIGOLD BIHARAMULO) Muhunda Nyakiloto amesema kampuni hiyo yenye wafanyakazi 228 kwa sasa lakini tangu ianzishwe mwaka 2013 imeshaajiri Watanzania 400 .

Amesema kuwa mgodi huo uko kwenye maonyesho hayo ili pamoaja na mambo mengine kuwaonyesha Watanzania kuwa sio lazima kuajiri wataalamu wa madini kutoka nje ya nchi yetu kwasababu mgodi huo umeajiri Watanzania wazalendo bila kuajiri mtaalamu kutoka nje ya nchi.

Na Mutta Robert -  Geita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post