Picha : WATU WENYE UALBINO WAFANIKIWA KUFIKA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO…WATOA DOLA ZAIDI YA 60,000 KUSOMESHA WATOTO WENYE UALBINO

Siku moja baada ya watu wenye ualbino kutoka katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania kushuka kutoka kileleni mwa Mlima Kilimanjaro kusikiliza ujumbe maalum wa watu wenye ualbino zaidi ya dola milioni 60 za Kimarekani zimekusanywa kwa lengo la kuwasaidia watoto wenye ualbino wanaoishi katika familia maskini kuendelea na masomo ya elimu ya juu.


Fedha hizo zimetokana na juhudi za watu wenye ualbino kupanda Mlima Kilimanjaro kwa muda wa siku 8 mfululizo na kupaza sauti zao kufikisha ujumbe juu ya changamoto zinazowakabili ikiwemo kukosa elimu bora.

Wadau wa haki za binadamu ambao wamepanda Mlima Kilimanjaro wakiambatana na watu wenye ualbino wamesema changamoto iliyosikika katika ujumbe uliotolewa mlimani imewagusa na kufanya changizo ili angalau kusaidia wachache kama alama ya ukombozi kwa watu wenye ulemavu.

Baadhi ya walengwa ambao wamefaidika na changizo hilo akiwemo Maria Mabula msichana ambaye amelelewa katika kituo cha Buhangija na kusoma katika shule ya msingi jumuishi Buhangija wamesema wamepata faraja kutokana na changizo hilo.

Nae mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino mkoa wa Kilimanjaro Simon Lymo ameiomba serikali kutoa msamaha wa ada kwa watu ulemavu kwa lengo la kusaidia kuondokana na utegemezi.

Kwa upande wake Monica Samwelson ambaye ni mwanahabari kutoka nchini Sweeden aliyeambatana na waandishi wengine kutoka nchi za bara la Afrika na Frank mshana wa kituo cha Utangazaji cha ITV walifanikiwa kufika kileleni na kuwakilisha vyema wanahabari wengine ambapo wanahabari wameshauriwa kuendelea kuibua changamoto za watu wenye ualbino kwa kuwa bado viutendo vya ukatili vinaendelea chini kwa chini na idadi ya watoto wenye ualbino barani Afrika kupotea pasipojulikana inaendelea kuongezeka.

Nao Lisa Lutchenberg,Vedastus Wilifred na Hugio ambao ni watu wenye ualbino kutoka katika mataifa mbalimbali wamesema changamoto ya watu wenye ualbino inasababishwa na umaskini uliokithiri katika jamii na tamaa ya kujipatia mali hivyo iko haja ya viongozi wa bara la Afrika kuendelea kushirikiana na raia wema kupambana na hali hiyo kwa kuwa kwa mtizamo tu na muonekano wa wazi inaonekana tofauti kubwa kati ya watu wenye ualbino wa bara la Afrika na mataifa mengine ya Ulaya.
Watu wenye ualbino kutoka mataifa mbalimbali wakiwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro - PICHA ZOTE NA FRANK MSHANA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post