WAWILI WAKAMATWA KWA KUMCHOMA MTOTO MOTO KWENYE MAKALIO

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wawili Judith Amoni Mwansansu (39) Mkazi wa Mwanjelwa na Aive Alex Swalo (17) Mkazi wa Mwanjelwa Mtaa wa Soko kwa kosa la kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto aitwaye Daines Kefas Mwansasu (06) Mwanafunzi wa Shule ya Awali – Mlimani na Mkazi wa Mtaa wa Soko hapa Jijini humo.


Taarifa ya tukio hilo imetolewa jana tarehe 1 Agosti, 2018 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Ulrich Matei.


Akielezea kuhusu tukio hilo kwa wanahabari, Kamanda Matei amesema tukio hilo lilifanyika Jumanne majira ya saa tatu usiku ambapo jeshi la polisi lilipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa raia wema, ya kwamba mtoto huyo amejeruhiwa sehemu mbalimbali kwa moto.


“Inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio mhanga alikuwa ameenda kucheza na rafiki zake na aliporudi nyumbani majira ya jioni ndipo shangazi yake alimuadhibu kwa kumchapa na waya wa umeme sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha na maumivu makali mwilini. Inadaiwa kuwa tarehe 01.08.2018 majira ya asubuhi, watuhumiwa waliendelea kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto huyo kwa kumuunguza kwa moto sehemu za miguuni na kwenye makalio,” ameeleza Kanada Matei.


Kamanda Matei amesema kuwa “Mtoto amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kufanyiwa vitendo vya ukatili na shangazi yake akishirikiana na mtoto wake. Watuhumiwa wote wawili wamekamatwa kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo. Mhanga amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi ya kitabibu.”


Katika hatua nyingine, amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu na ajali za barabarani ili kuhakikisha kuwa wageni na wakazi wa Mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao.


“Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa usalama hali inayopelekea kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu pamoja na ajali za barabarani,” amesema.


Kamanda Matei ameendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahalifu. Pamoja na kwa wazazi/walezi kujiepusha na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wao kwani ni kinyume cha sheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527