HALIMA MDEE NA WENGINE 13 WAKAMATWA NA POLISI

Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Halima Mdee (Mb) pamoja na viongozi wengine, wanachama na wapenzi wa CHADEMA Jimbo la Kawe takribani 13, jana walikamatwa na Jeshi la Polisi Kituo cha Polisi Kawe kwa kosa la kufanya mkusanyiko usio na kibali.

Mdee amesema alipigiwa simu na vijana wanaofanya biashara ya kutengeneza bustani wa eneo la Mzimuni, Kawe kwamba wamepewa notisi ya kuondoka.

Amesema wakati anapigiwa simu, alikuwa Kunduchi katika ziara hivyo ikamlazimu kwenda kuwasikiliza wananchi wake.

“Nilipofika, nilizungumza nao na kuwaeleza suala hili nalishughulikia, kwani nimewasiliana na wizara ya ardhi, mipango miji na Tarura (wakaka la wabarabara za vijijini na mijini).”

“Ni kweli wale vijana wako eneo la barabara na wamenieleza hawana tatizo la kuondoka, lakini wanahitaji kuelekezwa wapi watakwenda kuendelea na shughuli zao.” amesema.

Amesema baada ya kumaliza kuzungumza nao, aliondoka lakini alipofika mbele akaelezwa kuna watu wamekamatwa huko alipotoka.

“Nikaona nirudi, nilipofika nikakuta baadhi ya wafanyabiashara na wanachama wanarushwa kichura chura, nikahoji kuna nini sikupata majibu yanayoeleweka.”amesema.

Mdee amesema baada ya hapo, watuhumiwa hao waliokuwa chini ya ulinzi, wakapelekwa kituo cha polisi Kawe na yeye akatangulia kituoni.

“Nilipokuwa nakwenda, kama mita 20 nikaambia na mheshimiwa rudi, niliporudi nikaambiwa niko chini ya ulinzi, na kuniweka katika gari yao, tukaenda hadi kituoni na kuhojiwa kwa kufanya mkusanyiko usiokuwa na kibali,” amesema Mdee

Hata hivyo, baada ya kuhojiwa wale wafanyabiashara na wanachama wa Chadema waliachiwa huru.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527