MFANYABIASHARA AKAMATWA ASKARI WA UHAMIAJI DAR


Mfanyabiashara Davis Mosha anashikiliwa na Idara ya Uhamiaji baada ya jana Agosti Mosi, 2018 kukamatwa kwa madai ya kuwazuia askari wa Idara hiyo kutekeleza majukumu yao.


Akizungumza na MCL Digital leo Alhamisi Agosti 2, 2018 msemaji wa idara hiyo, Ali Mtanda amesema Mosha aliwashambulia askari hao na kumnyang’anya mmoja wao simu ya mkononi baada ya kufika katika jengo la Delina lililopo Sinza Mori, jijini hapa.


"Askari walifika kwenye majengo hayo na kujitambulisha kwa mlinzi na moja kwa moja walionyeshwa ofisi za meneja,” amesema Mtanda.


“Wakati wakifanya mazungumzo ya kikazi na meneja huyo, ghafla akatokea Mosha na kuanza kuwafokea, kisha kuwashambulia na kumnyang'anya askari mmoja simu yake.”


Amesema alichofanya Mosha ni kinyume cha sheria ya uhamiaji namba 54 kifungu cha 45 kipengele 1 F, kinachozungumzia kumzuia ofisa wa uhamiaji kufanya kazi yake ya ukaguzi.


Mtanda amesema bado wanamshikilia Mosha kwa uchunguzi zaidi na kama kuna hatua nyingine zitafuata watatoa taarifa.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo amesema tayari wamepokea taarifa ya tukio hilo, wanafanya uchunguzi kwa hatua za kisheria.


"Tunachunguza ili kujua kilichotokea ni nini, baada ya hapo ndio hatua nyingine zitafuata,” amesema Murilo.


Na Beatrice Moses, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527