MBUNGE WA CHADEMA,MWANDISHI WA HABARI NA WENGINE 14 WAACHIWA NA POLISI TARIME

Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima Sitta Tuma na wafuasi wengine 14 wa Chadema waliokuwa wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mkutano usio halali wameachiwa.

 Hata hivyo, wametakiwa kuripoti polisi kesho.

Matiko, Tuma na wafuasi hao walikamatwa na polisi jana wakati wa kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Turwa.

Akizungumza na wanahabari leo Agosti 9 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime /Rorya Henry Mwaibambe amesema polisi iliwataka wafuasi hao na viongozi watawanyike kwa kuwa mkutano huo siyo halali.


Pia, amesema baadhi ya wananchi waliondoka lakini wengine walikaidi, ndipo polisi ikalazimika kuwatawanya kwa mabomu lakini watuhumiwa hao walikaidi kuondoka jambo lililolazimu polisi kuwakamata.


“Nilipokea barua jana kutoka kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Turwa ya kusitishwa kwa kampeni za chaguzi za Chadema lakini chama hicho kilikaidi licha ya kupewa barua ya kusitisha mkutano.


“Polisi tulipewa barua ya zuio la mkutano ikionyesha kuwa Chadema wamekiuka kifungu cha 124 A cha Sheria ya Taifa ya uchaguzi,kamati ya maadili ya uchaguzi Kata ya Turwa kupitia kikao kilichoketi Agosti 8,2018 kilichowashirikisha na viongozi wa siasa kilisitisha kampeni za Chadema,” ameongeza.


Amesema Chadema waliambiwa wasifanye mkutano tangu saa sita mchana jana lakini saa kumi jioni kundi la watu zaidi ya 300 walionekana ofisi ya Chadema wakiwa kwenye mkusanyiko.


Mwaibambe amedai mbunge Matiko alitakiwa kuondoka eneo hilo lakini aligoma na kuanza kutukana polisi na hakuna yeyote aliyepigwa wakati wanakamatwa na kupandishwa kwenye gari.


“Kama wamepigwa wakiwa ndani ya kituo hiyo ni ishu,” amesema.


Akizungumzia kukamatwa kwa mwandishi wa habari Mwaibambe amesema;


“Nimepigiwa simu nyingi na media nyingi, waandishi wa habari wakiwamo wa Tarime wakiomba nimwachie Mwandishi mwenzao lakini polisi tumekataa, huyu amekamatwa akiwa kwenye mkusanyiko uliozuiwa. Waandishi wenzake waliondoka yeye akabaki.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527