MAMBO USIYOYAJUA KUHUSU MAREHEMU KING MAJUTO


Yakiwa yamepita masaa kadhaa tokea msanii wa vichekesho nchini, Alhaji Amri Athuman 'King Majuto' kufariki dunia siku ya jana, Agosti 8 2018 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alikuwa akipatiwa matibabu, watu mbalimbali wametoa salamu zao pole kutokana na kuguswa na msiba huo.

Taarifa ya msiba wa Mzee wa Majuto umegusa watu wengi kutoka ndani ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, kutokana na uhodari na umahiri wa kazi za sanaa alizokuwa akizifanya na kukubalika kwa jamii yote kuanzia watoto hadi wazee.

Alhaji Amri Athuman alizaliwa mwaka 1948 jijini Tanga na kusoma shule ya Msambweni iliyoko mkoani Tanga mwaka 1959 hadi 1965, ambapo alianza sanaa ya kuigiza kwa mara ya kwanza mwaka 1958 akiwa kwenye majukwaa mbalimbali.

Katika enzi za uhai wake Mzee Majuto aliwahi kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu kwa kujitolea akiwa na umri wa miaka 17, ambapo alipata nafasi hiyo kwa kuteuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga enzi hizo marehemu Issa Mtambo.

Baada ya kufikisha miaka 18, Mzee Majuto alichaguliwa kwa mara nyingine kujiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kambi ya Twalipo iliyopo maeneo ya chuo cha Uhasibu jijini Dar es Salaam na ilipofika mwaka 1972 aliachana rasmi na masuala ya jeshi na kufanya kazi za kijamii.

Mzee Majuto ndiyo msanii wa kwanza nchini Tanzania kuandaa na kuuza kazi zake za sanaa kupitia mikanda iliyokuwa inafahamika kwa jina la 'VHS' enzi hizo, na hadi umauti unamfika (kifo) ameshiriki zaidi ya kazi 89.

Mbali na kipaji cha uigizaji, Mzee Majuto pia ni mtunzi, mwandishi wa mswada pamoja na muongozaji filamu.

Marehemu Mzee Majuto ni miongoni mwa wasanii walioweza kufanikisha ndoto za vijana wengi waliokuwa na nia ya kutaka kufanya sanaa ya kuigiza, na kupitia yeye kwa namna moja ama nyingine waliweza kufahamika na kufanikiwa yale waliyokuwa wameyakusudia.

Septemba 24, mwaka 2015, Mzee Majuto alifanikiwa kuenda kufanya ibada ya 'Hija' kwenye mji wa Makka nchini Saudia Arabia na kunusurika kifo kufuatia ajali iliyotokea ya winchi kuanguka na kuua zaidi ya watu 109 na kujeruhi mahujaji 816.

Baada ya tukio hilo, Mzee Majuto ilipofika Mei 2 mwaka 2016 alitangaza rasmi kuachana na kazi ya uigizaji na kwamba anataka kumtumikia Mungu na kuomba asamehewe makosa kwa yale aliyotenda nyuma na kutangaza tena nia hiyo mwaka huu 2018 alipotoka nchini India kwa matibabu.

Jina la Mzee Majuto limeshindwa kupata thamani halisi ya kutokana na watu wengi walikuwa wanamtumia Mzee huyo kwa manufaa yao binafsi bila ya hata kumuangalia yeye namna ya kumuwezesha kiuchumi hususan katika sekta ya kilimo ambapo enzi za uhai wake alikuwa akipigania sana.

Itakumbukwa mnamo Oktoba 27, 2017, Waziri wa Habari, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe alikiri mbele ya umma kuwa Mzee Majuto amedhurumiwa pesa milioni 25 na kampuni ya filamu ambayo jina lake amelihifadhi na kudai atatumia hata mshahara wake kuhakikisha anawafunga watu hao.

Mwili wa marehemu Alhaji Amri Athuman maarufu kama King Majuto unatarajiwa kusaliwa katika msikiti wa Muhimbili leo asubuhi na kisha kupelekwa katika uwanja wa Karimjee kwa ajili ya kupewa heshima za mwisho, kabla ya kuelekea Mkoani Tanga kuzikwa katika mashamba yake.

Pumzika kwa amani mzee Majuto.

Imeandaliwa na EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527