MTOTO WA MIEZI MITANO AUAWA KWA KULISHWA SUMU NA BABA YAKE MBEYA


JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanaume mmoja mkazi wa Kijiji cha Isitu Wilayani Mbarali ambaye amefahamika kwa jina la GEOFREY EMILIO  MWANGANGA [21] kutokana na kumuua mtoto wake aitwaye PRINCE GEOFREY EMILIO mwenye umri wa miezi 5.

Mwili wa marehemu ulipatikana mnamo tarehe 30.08.2018 majira ya saa 17:30 jioni huko katika Kijiji cha Isitu porini, Kata ya Chimala, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimuua mtoto huyo kwa kumnywesha sumu ambayo bado haijafahamika aina yake na kisha kwenda porini kumfukia. 

Inadaiwa kuwa awali mnamo tarehe 28.08.2018, baba mzazi wa marehemu bwana GEOFREY EMILIO alikwenda nyumbani kwa mke wake ambapo alikuwa anaishi baada ya kuwa wametengana na kumchukua mtoto huyo kwa nguvu bila kibali cha mama mzazi wa mtoto.

Mtuhumiwa baada ya kukamatwa alidai kuwa mtoto alikuwa amempeleka kwa ndugu zake huko Makete Mkoani Njombe lakini baadae alikiri kuwa mtoto huyo amemuua na kumtupa porini na katika ufuatiliaji aliwapeleka Polisi eneo alipokuwa amemfukia marehemu.

Chanzo cha tukio hili ni wivu wa kimapenzi kwani mtuhumiwa alikuwa anahisi mtoto huyo sio wake amebambikiwa ni wa mwanaume mwingine. 

Mwili wa marehemu umefukuliwa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Misheni Chimala kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kitabibu.

Katika Tukio Jingine:
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawasaka watu wanaodaiwa kufukua kaburi na kisha kuchukua mifupa ya mwili wa marehemu ambaye alikuwa na ulemavu wa ngozi [Albinism].

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 30.08.2018 majira ya saa 03:00 usiku huko katika Kijiji cha Ngonga kilichopo Kata ya Ngonga, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa mbeya ambapo kaburi la mtu mmoja aliyekuwa anajulikana kwa jina la ANDUSAMILE MWALWEBE @ KANJANJA [65] Mkazi wa kijiji cha Ngonga ambaye aliyefariki dunia mwaka 2012 kwa maradhi ya kawaida na ambaye aliyekua na ulemavu wa ngozi (Albinism) kukutwa limefukuliwa na mtu/watu wasiojulikana na kisha watu hao kuchukua mifupa ya mwili wa mtu huyo ( skeleton).

Kiini cha tukio hilo ni imani za kishirikina. Aidha inadaiwa kuwa kabla ya

kuchukua mifupa ya marehemu, watu hao walichimba shimo kubwa pembeni mwa kariburi hilo lililojengwa kwa tofali za saruji kisha wakabomoa upande mmoja wa jeneza (sanduku) na kuchukua mifupa hiyo na kutoweka nayo. Upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na msako ili kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa hao.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na misako na operesheni

mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ili kuzuia na kudhibiti matukio ya uhalifu pamoja na ajali za barabarani

Imesainiwa na.
[MODESTUS CHAMBU – ACP]
KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
KAIMU KAMANDA: 0658 376 052

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post