STEVE NYERERE APIGWA BENCHI MSIBA WA KING MAJUTO

Muigizaji Steve Nyerere ambaye amekuwa mstari wa mbele kuwaunganisha wasanii hasa katika kipindi cha misiba au matatizo yanayowatokea wasanii wenzao, amepigwa benchi kwenye msiba wa Mzee Majuto.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuundwa kamati ya kushughulikia msiba huo ambayo imeundwa na Chama cha waigizaji Mkoa wa Kinondoni (TDFAA) pamoja na chama cha waigizaji Taifa.

Kuondolewa kwa Steve ni kutokana na kutokuwa mwanachama wa TDFAA, hivyo hawezi kuteuliwa katika kamati.

Mara baada ya Mzee Majuto kufariki, wajumbe wa kamati wakiongozwa na Simon Mwakifamba walifika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya taratibu za kuhifadhi mwili na wakatoa tamko kwamba taratibu zote za kuaga zitafanyika Muhimbili na baadaye kusafirisha kwenda Donge, jijini Tanga kwa maziko.

Wakati hayo yakiendelea Steve Nyerere alifika Muhimbili saa 6.05 usiku, akija na utaratibu mwingine kuwa shughuli za kuaga zifanyike kwenye viwanja vya Karimjee kwa kuwa Majuto ni mtu maarufu na tayari walishaanza kukaa kikao na wasanii wenzake kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kuagiwa kwenye viwanja hivyo.

Hata hivyo, alipotoa wazo hilo, mmoja wa wanandugu alijitambulisha kwa jina la Ashraf, alimwambia kuwa lazima wawasiliane na ndugu wengine kwa hatua hiyo.

Pamoja na wazo hilo kukubalika, Nyerere alibaki pembeni na hata alipoulizwa zaidi kuhusu utaratibu alikataa kwa kuwa si mwanakamati wa kamati ya maziko

“Mimi sihusiki na chochote kwani nimekuwa nikitukanwa kwamba nakusanya fedha za rambirambi kisha nazitafuna,” anasema.

Mzee Amri Athumani aliaga dunia jana majira ya saa 2:00 usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa akitibiwa.


Na Rhobi Chacha, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527