
Hii ni Taarifa iliyotolewa jana Agosti 22 na Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene
Hatimae fomu ya rufaa ya Mgombea Ubunge Jimbo la Korogwe Vijijini kupitia CHADEMA, Bi. Amina Ally Saguti imepokelewa na Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Korogwe, Ndugu Frolian Kimaro baada ya malumbano marefu, ambapo mamlaka zinazohusika zilikuwa zimekataa kuipokea.
Katika rufaa hiyo Mgombea Bi. Saguti anapinga, pamoja na masuala mengine, uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Korogwe Vijijini kumtangaza mgombea ubunge wa CCM kuwa amepita bila kupingwa, huku kukiwepo na ukiukwaji mkubwa wa taratibu zinazosimamia uchaguzi nchini.
Hadi mwisho wa kupokea rufaa hiyo ulipokuwa unakaribia jioni hii, kwa mara nyingine tena uteuzi wa mgombea huyo wa CHADEMA ulikuwa bado unawekewa vikwazo baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kukataa kupokea fomu hiyo tangu mchana.
Mgombea huyo akiambatana na Viongozi wa CHADEMA Wilaya ya Korogwe, walifika ofisini kwa msimamizi leo mchana kuwasilisha fomu hizo lakini alikumbana na vikwazo hali iliyoonesha kuwa kuna dalili za kuhakikisha uamuzi wa juzi haubadiliki ili CCM ipite bila kupingwa katika jimbo hilo.
Fomu hiyo na. 12 ilipatikana kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya Uongozi wa CHADEMA ngazi ya taifa kulazimika kufanya mawasiliano ili kupata fomu hiyo kutokana na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Korogwe kukataa kutoa.
Chama tayari kimeshamwandikia rasmi Mkurugenzi wa NEC kumtaka achukue hatua za haraka kuingilia kati mwenendo wa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Korogwe hasa kubatilisha uamuzi wake uliokiuka taratibu zinazosimamia uchaguzi kwa kukataa kupokea fomu za kugombea za Mgombea wa CHADEMA na vyama vingine huku akimtangaza Mgombea wa CCM kupita bila kupingwa kinyume cha sheria na kanuni za uchaguzi.
Tumaini Makene
Social Plugin