MASHABIKI WA SIMBA WAMCHEFUA HAJI MANARA


Mashabiki wa Simba wakishangilia kwenye moja ya mechi za timu hiyo.

Baada ya Simba kuanza vema kwa ushindi kiduchu wa goli 1-0 jana dhidi ya Prisons, afisa habari wa klabu hiyo Haji Manara amewafungukia mashabiki wanao beza ushindi huo katika mechi yao ya ufunguzi wa Ligi kuu bara.

Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa mapema kabisa na Meddie Kagere mnamo dakika ya pili tu ya mchezo aliyesajiliwa kutoka Gor Mahia FC huku aliyekuwa straika wa Lipuli FC na sasa Simba, Adam Salamba kucheza takribani dakika 6 bila kufanya maajabu kama alivyozoeleka.

Manara kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii amefunguka kuwa anawashangaa wanaobeza na kulalamikia kiwango cha kocha wao na kudai kuwa hafai kukinoa kikosi hicho.

Manara ameandika; “Wakati mwingine najiuliza nini wanadamu wanataka? hasa washabiki wa mpira, nimetalii kidogo kwenye magroup machache ya wanasimba kwenye WhatsApp nimeshangaa baadhi yetu kutokuridhika na ushindi wa leo wa goli moja dhidi ya Prisons. Wengine kwenye Instagram wanafika mbali zaidi eti mfumo wa kocha haufai”.

Ameongeza kuwa “Mpira ni sayansi kubwa kuliko kwenda mwezini au daktari kumfanyia upasuaji wa kichwa mtu,ukubwa wa sayansi hii ni kwamba hujui mpinzani wako kajipangaje, hujui kama siku hyo wachezaji wako watacheza kwa kiwango gani lakini kubwa Sayansi hii haina jawabu la moja kwa moja kama hesabu au hisabati 3×3 ni tisa tu, hata ukokotoe vipi! Huku kwetu kwenye ndiki 3×3 inaweza kuwa bilioni nane”.

Baada ya Simba kuanza kwa ushindi huo jana, watani zao wa jadi Yanga, leo wanashuka dimbani kuwakaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja huohuo wa taifa saa 12 jioni, ambapo kuelekea mechi hiyo mwenyekiti wa kamati ya usajili na mashindano, Hussein Nyika, ameahidi kuwa Yanga itauwasha moto mkali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527