CHADEMA YATOA MSIMAMO HATMA YA MBOWE CHADEMA


Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe.

Baada ya kutolewa kwa taarifa kwamba Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe ndio chanzo cha Wabunge wawili kutimkia CCM hivi karibuni, Chama hicho kimetoa tamko na kueleza kwamba hakiwezi kupangiwa kubadilisha mwenyekiti wao na CCM au watu wanaondoka ndani ya chama hicho.

Tamko hilo limekuja siku kadhaa baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo la Ukonga Mwita Waitara, na mbunge wa Monduli Julius kulanga kudai kwamba moja ya sababu zilizowaondoa CHADEMA ni mgogoro kati yao na Mbowe kuendelea kung’angania nafasi ya uenyekiti ndani ya chama hicho, na kunyimwa kushirikikiana na serikali katika shughuli za maendeleo.

Akizungumza na www.eatv.tv katika mahojiano maalum, Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje- CHADEMA bwana John Mrema amesema watakaoamua kiongozi wao ni nani ni wanachama wa CHADEMA na viongozi wao kwa mujibu wa katiba ya Chama hasa ikifika nyakati za uchaguzi, hivyo kinachofanywa kwa sasa na wanasiasa hao ni propaganda.

Akiendelea jibu hoja ya aliyekuwa mbunge wa ukonga aliyetimkia CCM kwamba CHADEMA ni 'SACCOS' ya Mbowe, Mrema amemtaka Waitara kutoa sababu zilizomfanya akakimbia,lakini siyo hizo ambazo alizitaja kwa sababu Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) anakagua chama kila mwaka na kutoa ripoti yake ambayo inaonesha mapato, matumizi na mali za chama.

“Unapokuwa na kiongozi ambaye anashindwa hata kusoma ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali halafu anaishia kusema uongo kwa kweli ni fedheha, ni kiongozi ambaye unaona kabisa kwamba hakuwa amejiandaa kuwa kiongozi”. Amesema Mrema

Mwishoni mwa wiki iliyopita aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ukonga (CHADEMA) Mwita Waitara, alitangaza kujiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM akidai moja kati ya vitu vilivymuondoa ndani ya chama hicho ni ugomvi wake na Mbowe ndani ya chama,ambapo baadaye Mbunge wa Monduli –CHADEMA naye alijiunga na CCM kwa sababu zinazofanana na hizo.

Aidha katika kipindi cha takribani miwili na nusu tayari wabunge watatu wa CHADEMA wameshajivua nyadhifa zao, na kujiunga na CCM ambao ni dokta Godwin Mollel wa Sia, Mwita Waitara wa Ukonga pamoja na bwana Julius kalanga wa Monduli.
Theme images by rion819. Powered by Blogger.