STAND UNITED NA MWADUI FC KUONESHANA UBABE WIKI HII WAKITAMBULISHA WACHEZAJI WAPYA


Viongozi wa Stand United na Mwadui FC wakizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga leo. Wa kwanza kulia ni kocha wa timu ya Stand United Niyogabo Amars, akifuatiwa na Mwenyekiti wa Timu hiyo Dkt. Ellyson Maeja, Katibu wa timu ya Mwadui FC Ramadhani Kileo na Kocha wa Mwadui FC Bizimungu Ally. Picha na Marco Maduhu - Malunde1 blog
Timu za mpira wa miguu za mkoani Shinyanga Stand United 'Chama la Wana" na Mwadui Fc, zinatarajia kufanya bonanza la michezo (SHY DEARBY) la kutambulisha wachezaji wao waliowasajili kushiriki kucheza ligi kuu bara 2018/2019.

Timu hizo zinatarajia kufanya bonanza hilo siku ya Jumamosi Agosti 11,2018 katika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

Wakizungumza leo na vyombo vya habari mjini Shinyanga viongozi wawili wa timu hizo Stand United Dkt, Ellyson Maeja na Mwadui FC Ramadhani Kileo walisema mchezo huo wa kirafiki ni sehemu za maandalizi ya kuonyesha uwezo wa wachezaji wao waliowasajili hivi karibuni.

 Viongozi hao walisema wameamua kuungana kuwa kitu kimoja kama timu za mkoani Shinyanga ili kuwa na umoja ambao utawafanya kushika nafasi za juu ama kuchukua kombe kwenye msimamo wa ligi kuu bara (2018-19). 

Walieleza kuwa mbali na mchezo huo wa kirafiki kati ya 'Wapiga debe' Chama la Wana na 'Wachimba Madini ya Almasi' Mwadui FC pia wataendesha zoezi la uchangiaji damu ili kuondoa uhaba wa damu salama katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga. 

“Tumeamua kuendesha bonanza hili la uchangiaji damu pamoja na kupima Virusi vya Ukimwi, ikiwa ni moja ya mchezo wa kutambulisha wachezaji wetu wapya kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga, ambao ndiyo mashabiki wetu watakao tuunga mkono katika kuhakikisha timu zetu zinapata ushindi,”alisema Dkt. Maeja.

Naye katibu wa timu ya Mwadui FC Ramadhani Kileo, alisema uhasama uliokuwepo kwenye timu hizo mbili kama hapo awali haupo tena ,hivyo wao kwa sasa ni marafiki ambapo wameungana kuwa kitu kimoja na kutoa burudani kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga. 

Timu hizo mbili katika Msimu wa Ligi kuu bara uliopita Mwaka (2017-18) Mwadui Fc iliishia nafasi ya 11, huku Stand United ikishika nafasi ya 10. 

Na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527