AMBULANCE YA MIRUNGI YATUPA NJE WATATU....YUMO MGANGA MKUU ,DEREVA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Elias Ntiruhungwa amewasimamisha kazi watumishi watatu akiwemo kaimu mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya ya Tarime baada ya gari la wagonjwa la hospitali hiyo kukamatwa likisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi wilayani Bunda mkoani Mara Julai 11 Mwaka huu.

Waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mganga Mkuu (DMO) Dkt Innocent Kweka, Kaimu Mganga Mfawidhi Dkt Amir Kombo na katibu wa Hospitali Rwegasira Karugwa kutokana na uzembe waliofanya mpaka kitendo hicho kinafanyika.

“Namsimamisha kazi DMO, Mganga Mfawidhi na Katibu wa hospitali kuanzia leo hadi tutakapomaliza uchunguzi wetu ambao umeanza kubaini kwa nini gari la wagojnwa lilitumika kusafirisha madawa ya kulevya ,kama hawana hatia watarudi kazini”,alisema Mkurugenzi.

Ntiruhungwa amesema hawezi kuvumilia kitendo hicho ambacho kimechafua jina la Hamashauri yake na nchi kwa ujumla na kwamba yeyote ambaye atabainika kuhusika katika tukio hilo atachukuliwa hatua kali.

Ameongeza kuwa tayari suala hilo linafanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini dereva huyo George Matai alipataje fursa ya kusafirisha madawa ya kulevya kwa kutumia gari la wagonjwa na kusema kuwa tayari amemsimamisha kazi kuanzia leo.

“Huyu dereva alichokifanya ni kitu cha kushangaza sana na kuzidi kuaibisha taifa kwa ujumla lazima afukuzwe kazi kwa sasa tayari anashikiliwa na polisi na akitoka hata kama ni baada ya miaka 20 na kama sipo maandishi yapo atafukuzwa tu hatuwezi kufumbia macho suala hili”,alisema Mkurugenzi.


Mkurugenzi huyo aliwataka wakuu wa idara katika Halmashauri yake kutimiza wajibu wao kikamilifu ili kuepekuka vitendo vya aibu kama hivyo kutokea tena.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara (RPC) Juma Ndaki aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa dereva huyo na mtuhumiwa mwingine wanashikiliwa baada ya kukamatwa na shehena ya mirungi.
Na Frankius Cleophace Tarime.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527