KAULI YA JOKATE MWEGELO BAADA YA KUULAMBA U - DC


Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo.

Ikiwa ni siku moja baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo, amefunguka kuwa katika safari yake ya kisiasa kuna muda alitamani kukata tamaa. 


Jokate kupitia ukurasa wake wa Instagram amesema kuwa katika maisha ya siasa kuna wakati ulifika hakuelewa hatma yake kutokana na changamoto alizopitia na ilimpelekea kuelekea kukata tama kwakuwa alikuwa chini sana.

“Kuna muda mwaka jana mwishoni nilikuwa so down nilitamani kukata tamaa na kila kitu kwenye maisha nilikuwa pia sijaelewa vizuri hatma yangu kwenye siasa”, amesema Jokate na kuongeza kuwa,

“Unaweza ukawa unapitia mitihani migumu sana kwenye maisha yako lakini inakubidi usikate tamaa saa zingine kwasababu tu ya wale wanaokutegemea, wanaokuangalia na kuvutiwa nawe na kujifunza kupitia maisha yako. Lakini zaidi kwasababu safari ya mafanikio ina milima na mabonde, inabidi upambane na kiukweli hakuna mafanikio yasiokuwa na changamoto”, amesema Jokate.

Kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, Jokate alikuwa Kaimu Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), aliteuliwa kushika nafasi hiyo Aprili mwaka 2017 na akaondolewa kwenye nafasi hiyo Machi mwaka 2018.

Jokate pia amewahi kuwa mshindi wa pili katika mashindano ya ‘Miss Tanzania’ mwaka 2006, ambapo Wema Sepetu alishinda taji hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527