KANGI LUGOLA : NIMEUVAA UNINJA SITAMWONEA AIBU ANAYEHATARISHA AMANI YA NCHI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema hatamwonea aibu kiongozi au mtu yeyote atakayetaka kuhatarisha amani ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, amesema kuanzia sasa, wanaotaka kuhatarisha amani, wajue kwa sasa ameuvaa uninja usoni.

Waziri Kangi aliyasema hayo jana mjini Mbeya alipokuwa akizungumza na viongozi wa taasisi, mashirika, mamlaka na taasisi za Serikali pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkoa wa Mbeya.

Katika maelezo yake, waziri huyo aliwataka viongozi wajiandae kwa uamuzi mgumu atakaoutoa baada ya kupokea taarifa kutoka kwenye mamalaka husika zinazojihusisha na usalama barabarani.

“Nilipokuwa bungeni, kuna baadhi ya watu walionekana kutaka kuharibu amani na mimi kulazimika kuvaa kofia ya kininja ambayo ilikuwa ya kitambaa.

“Lakini, kwa sasa nitalazimika kuvaa kofia hiyo ya chuma na nzito zaidi kwani ninaopambana nao ni makamanda wenzangu.

“Niliapishwa Jumatatu wiki hii kushika nafasi hii inayoyahusisha majeshi ya magereza, uokoaji, idara ya uhamiaji, vitambulisho vya Taifa, wakimbizi, usajili wa vyama vya kijamii, makanisa na misikiti.

“Kwa kawaida, vyombo vyote hivyo ndivyo vinavyohakikisha amani ya nchi inakuwepo.

“Hivyo basi, wananchi wanapopata ajali mahali popote ikiwamo Mbeya na maeneo mengine ya nchi na wakati huo huo Serikali ikashindwa kuchukua hatua, basi nchi haitakuwa na amani wala utulivu.

“Kwa hiyo, sitanii bali nimeamua kuuvaa uninja nikimaanisha na sitamwonea haya mtu yeyote."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527