Thursday, July 5, 2018

BOSI WA MABASI YA ZACHARIA ANYIMWA DHAMANA KESI YA KUJARIBU KUUA MAAFISA USALAMA WA TAIFA

  Malunde       Thursday, July 5, 2018


Mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa mabasi ya Zacharia, Peter Zacharia

Mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa mabasi ya Zacharia, Peter Zacharia amepandishwa Mahakamani na kusomewa mashitaka mawili ya kujaribu kuua maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa kwa kuwapiga risasi.

Hayo yamebainishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Musoma hii leo Julai 05, 2018 na kumnyima dhamana mtuhumiwa huyo kwa kile kilichoelezwa kwamba wale waliojeruhiwa hali zao kiafya kuwa ni mbaya katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo wanapatiwa matibabu.

Mbali na hilo, Mahakama imesema sababu nyingine za mtuhumiwa huyo kutopewa hati ya dhamana ni kutaka kulinda usalama wake lakini Mawakili wa upande wa utetezi wakapinga hoja hiyo kwamba hakuna ukweli wowote kama mteja wao akiachiwa ataweza kudhurika. 

Vile vile, Mawakili wa upande wa utetezi wamesema hakuna hati yoyote iliyowasilishwa Mahakamani ya kuonesha kwamba hao majeruhi wamelazwa katika hospitali ya Muhimbili na kama kweli wametibiwa.

Baada ya mvutano huo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Musoma, Rahim Mushi amesema Mahakama ipewe muda mpaka Julai 10 ili waweze kupitia uamuzi mdogo kuhusiana na suala la dhamana kama mtuhumiwa anastahili au laa.

Peter Zacharia alikamatwa na Jeshi la Polisi mnamo Juni 29, 2018 akidaiwa kuwajeruhi kwa risasi watu wanaodaiwa kuwa ni maofisa Usalama wa Taifa, tukio lililotokea katika kituo cha mafuta kinachomilikiwa na mfanyabiashara huyo.
Chanzo- EATV
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpyaHAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.bdkxfuvweev_drskoew
Previous
« Prev Post