Makubwa Haya : JAMAA ANG'ANG'ANIA JUU YA PAA LA KANISA


Mkazi wa Nyankumbu mjini Geita, Bernadino Kasambula ameweka makazi yake kwenye paa la kanisa kwa siku nne mfululizo akidai ni nyumba ya familia yake.

Kasambula na ndugu zake wanne walikuwa wakitumikia vifungo tofauti jela – yeye na nduguye mmoja miaka 30 na wengine wawili vifungo vya maisha – amedai kuwa amechukua hatua hiyo baada ya kutoka gerezani na kukuta mashamba yao na nyumba vimeporwa na wao kukosa mahali pa kuishi.

Akizungumza leo Juni 5,2018 Bernadino amesema hatashuka mpaka Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel atakapofika na kusikiliza kilio chao.

Kasambula amedai kuwa licha ya eneo lao kuwa na makaburi ya wazazi wao waliofariki wakiwa gerezani, lakini mtu anayelimiliki sasa amekataa kurudisha ardhi yao ambayo alidai ni mali ya wazazi wake.

Kasambula na ndugu zake hao walifungwa mwaka 1986 na yeye na ndugu yake waliyekuwa wakitumikia miaka 30, walimaliza kifungo chao na mwingine mmoja aliachiwa Desemba 9 mwaka jana kwa msamaha wa Rais huku akidai kwamba mwingine amefariki dunia.

Ndugu hao wanne walihukumiwa vifungo hivyo baada ya kupatikana hatia ya kosa la mauaji.

Ndugu wa Bernadino ambaye alifungwa kifungo cha maisha, Joachim Kasambula alisema eneo hilo ni moja ya mashamba matatu ambayo yameporwa wakati wakiwa wanatumikia kifungo.

“Kila tunapodai mali yetu tumekuwa tukitishwa lakini wanaoweza kutusaidia ni Mungu, Rais John Magufuli na mkuu wa mkoa, Gabriel,” amesema.

Mmoja wa majirani, John Joseph alisema baada ya ndugu hao kufungwa, wazazi wao walihama mwaka 1987.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyankumbu, Simon Duda amesema Bernadino alianza kulalamika kuanzia mwaka 2016 alipotoka gerezani na alifungua kesi katika baraza la ardhi ambayo iliamuru pande zote mbili kugawana eneo hilo.

Amesema hata hivyo upande unaomiliki sasa ulipinga na kufungua kesi katika Mahakama ya wilaya ambayo ilifuta hukumu ya baraza la ardhi na kutoa ushindi kwa familia inayomiliki eneo hilo sasa.

Deusdedit Bupamba, mtoto wa Helena Bujimu anayedaiwa kumiliki eneo hilo kwa sasa, alidai kuwa mama yake alilinunua kutoka Kwa John Kingi mwaka 1987 na kuwataka wanaolalamika kukata rufaa mahakamani kama hawaridhishwi na hukumu iliyotolewa.

Na Rehema Matowo, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527