KASEJA AFUNGUKA MIPANGO YAKE BAADA YA KUSTAAFU SOKA


Mlinda Mlango mkongwe nchini aliyesajiliwa na klabu ya KMC ya Dar Es Salaam, Juma Kaseja amefunguka kuwa kwa sasa hajaamua nini cha kufanya katika maisha yake nje ya Soka hadi hapo atakapostaafu rasmi.

Kaseja amefunguka hayo katika kipindi cha KIPENGA XTRA kinachorushwa na East Africa Radio ambapo baada ya kuulizwa kuhusu mipango yake baada ya kustaafu soka alisema kuwa kuna kazi nyingi za kufanya katika maisha nje ya Soka tofauti na wachezaji wengi wanavyofikiria.

“Kikubwa ninachotaka kusema ni kwamba maisha yangu yote mimi nilikuwa ndani ya Mpira nimecheza na mpaka sasa hivi bado nacheza kwa hiyo nitaamua baada ya kutoka kwenye Mpira niende wapi kwa sababu naamini kuna vitu vingi naweza nikafanya au kazi nyingi naweza nikafanya na maisha yangu yakaendelea kuwepo “. Alisema Kaseja 

Aliwaasa Walinda Mlango wanaochipukia kuwa na nidhamu na bidii ya kazi ili waweze kufikia katika nafasi ambazo yeye na walinda Mlango wengine wakubwa waliwahi kuzifikia.

Pia Kaseja aliongeza kuwa maisha ya mchezaji akiwa anacheza Soka ndiyo yatakayoamua maisha yake baada ya kutoka katika Soka, endapo mchezaji ataishi vibaya kipindi anacheza Soka basi maisha yake yatakuwa vibaya tuu baada ya kustaafu.

Mkongwe huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) ambayo imepanda ligi kuu Tanzania Bara msimu ujao baada ya kuachana na Kagera Sugar ambayo ameielezea kuwa imemuheshimu na kumthamini kwa kipindi chote alichohudumu katika klabu hiyo.
Chanzo- EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527