POLISI YAKAMATA MATAPELI 15 WA SMS ZA 'ILE PESA ITUME KWENYE NAMBA HII'...


Watu 15 wamekamatwa na Jeshi la Polisi wakituhumiwa kutuma ujumbe kwa watumiaji wa simu kwa lengo la kutapeli fedha watu.

 Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari leo Jumatano Juni 27,2018 Jumatano, Kaimu Kamanda Kanda Maalumu Dar es Salaam Liberatus Sabas amesema kuwa watu hao wamekamatwa katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam pamoja na Sumbawanga, Rukwa.

Ameeleza kuwa pamoja na watu hao 15, Jeshi hilo limekamata simu 45, kadi za simu 352 ambazo hazijasajiliwa kwa majina yao, vitambulisho mbalimbali pamoja na kompyuta mpakato tano.

Kamanda Sabas ameongeza kuwa watu hao wamekiri kuhusika na wizi huo wa kimtandao na kueleza kuwa walikuwa wakitumia mfumo ujulikanao kama BackSMS kutuma jumbe hizo fupi.

“Kupitia mfumo huo, walikuwa wanaweza kutuma sms 10,000 kwa wakati mmoja za meseji hizo za kuomba pesa,” aliongeza. 

Kamanda Sabas amesema kwamba uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini watu wengine wanaohusika na utapeli wa aina hiyo.
Chanzo- Habarileo
Theme images by rion819. Powered by Blogger.