Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Warajis Wasaidizi wa Mikoa na Maafisa
Ushirika wa Halmashauri za Wilaya nchini wakutane na wadau wa vyama vya
msingi vya zao la kahawa na wapitie upya tozo zilizo kwenye zao hilo.
Amesema
tozo nyingi haziko kisheria bali zinawekwa na vyama vya msingi na
zimelenga kuwanyonya wakulima badala ya kuwasaidia kuinua vipato vyao.
Ametoa
kauli hiyo jana Mei 19, 2018, wakati akizungumza na Warajis Wasaidizi
wa Ushirika wa Mikoa 25 na Maafisa Ushirika wa Halmashauri za Wilaya 140
zinazolima mazao makuu ya biashara yaani kahawa, chai, tumbaku, pamba
na korosho.
Walikuwa
kwenye kikao alichokiitisha jijini Dodoma ili kujadili namna bora ya
kuongeza uzalishaji wa mazao hayo na kufanya ufuatiliaji wa maagizo
ambayo alikwishayatoa kwenye ziara zake mikoani.
Tangu
mwaka jana, Waziri Mkuu ameshafanya vikao zaidi ya sita na wadau wa
pamba, korosho, tumbaku na kahawa nchini ili kubaini namna bora ya
kufufua mazao hayo makuu.
Akizungumzia kero ya tozo za mazao kwa wakulima, Waziri Mkuu alisema:
“Kuna
tozo nyingi zinazowekwa na vyama vya msingi na hazina uhalali wowote;
tozo nyingine si za vyama vikuu, bali ni za AMCOS tu (vyama vya
msingi).”amesema