WAPINZANI WA YANGA WATUA BONGO

Wapinzani wa Yanga SC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, Rayon Sport ya Rwanda wamewasili mchana wa leo Mei 14, 2018 tayari kwa mtanange huo wa Kundi D utakaopigwa Jumatano ya wiki hii katika dimba la Taifa, Jijini Dar es Salaam.

Timu ya Rayon inatarajiwa kufanya mazoezi yake ya mwisho siku ya kesho Jumanne katika kiwanja cha Taifa kabla ya kukutana na wenyeji wao katika mtanange wenyewe ambao kila mmoja anatamani kupata matokeo mazuri ili azidi kujiweka sawa katika hatua za mbele. 

Aidha, waamuzi wa mchezo huo nao wamewasili leo wakiwa wametokea Angola akiwemo Helder Martins De Carvalho atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Ivanildo Meirelles De O Sanche Lopes na Wilson Valdmiro Ntyamba.

Kwa upande wa Yanga, wanarejea leo Jijini Dar es Salaam kutokea Morogoro ambako jana Mei 13, 2018 walicheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kufungwa bao 1-0 na wenyeji, Mtibwa Sugar uwanja wa Jamhuri. 
Kwa upande mwingine, viingilio katika mchezo huo vimepangwa kuwa ni shilingi. 15,000 kwa VIP A, 7,000 kwa VIP B na C na 3,000 kwa mzunguko.
Theme images by rion819. Powered by Blogger.