Picha : POLISI SHINYANGA WAFANYA MAZOEZI YA KUKABILIANA NA UHALIFU.. 'ANDAMANA ILE KWAKO'

Jeshi la polisi mkoani Shinyanga  limefanya mazoezi ya utayari wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu ‘Police Force Show Off’.

Akiongoza mazoezi hayo leo Jumatano Aprili 25,2018 majira ya saa 2 hadi saa 4 asubuhi, Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule alisema mazoezi hayo ni ya kawaida kwa ajili ya kujiweka tayari kukabiliana na uhalifu unaoweza kujitokeza ili kulinda raia na mali zao.

“Kwa utaratibu wetu wa kawaida au kalenda yetu ya kazi jeshi la polisi kama Taasisi mojawapo kubwa mkoani Shinyanga linatakiwa kila baada ya muda fulani lazima lifanye kitu ambacho kitaalamu wanaita Emergency Exercise Drill ili kupima uwezo wa askari wake (Police Personnel) lakini pia pamoja na raslimali vifaa tulivyonavyo ikiwemo Magari, pikipiki, Radio za mawasiliano, wanyama mbwa wa doria na kadhalika”,alieleza Kamanda Haule.

“Lengo ni kujitazama ama kuangalia tuna uwezo kiasi gani katika kukabiliana na matukio makubwa ‘crisis’ yanayo weza kujitokeza mfano matukio makubwa ya uhalifu wa kijinai,majanga makubwa kama ya moto, mafuriko maporomoko ya udongo, tetemeko la ardhi ama ajali kubwa zinazohusisha vifo na majeruhi wengi kwa pamoja”,aliongeza

Kamanda Haule alitumia fursa hiyo kuwataka wakazi wa Shinyanga kuachana na mpango wa kuandamana siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26,2018.

“Jeshi la polisi katika mkoa wa Shinyanga halitaki kusikia kuwa kuna hata chembe ya maandamano hayo haramu,Naungana na mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack kupinga kwa nguvu zote maandamano hayo haramu yaliyokusudiwa kufanywa na watu ambao naweza kuwaita si wastaarabu,katika hili tunawaambia kabisa wananchi bora tupate lawama kuliko fedheha”,aliongeza Kamanda Haule.

Kuelekea kwenye maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 Aprili 2018,tayari Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ametoa onyo kali kwa watu waliopanga kufanya maandamano siku hiyo aliodai wanashinikizwa na watu wanaoishi nje ya Tanzania.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule  akitoa maelekezo wakati wa mazoezi
Askari polisi wakifanya mazoezi
Askari polisi wakiwa katika gari la maji ya kuwasha
Askari polisi wakiwa katika magari
Askari wakipita mtaani






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527