Monday, April 2, 2018

MAASKOFU WAWILI WAWAPINGA WENZAO WA KKKT NA KATOLIKI

  Malunde       Monday, April 2, 2018
Maaskofu wawili wamepinga matamko yaliyotolewa hivi karibuni na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).


Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani na Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kibaptisti Tanzania, Michael Nhonya, wamesema viongozi wa dini wanatakiwa kubaki kuwa walezi, washauri, wakemeaji, wenye kuonya na kuelimisha jamii ili Watanzania waendelee kuishi kwa umoja na amani na kuwataka wajipime wanapelekaje ujumbe wao wa kinabii kwa viongozi wao.


Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani amepingana na matamko yaliyotolewa na viongozi wa dini kuhusu mwenendo wa Serikali iliyoko madarakani.


Akihubiri katika ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Roho Mtakatifu mjini Dodoma, Askofu Chilongani alisema, “Hivi karibuni kumekuwa na matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa madhehebu ... Sipo hapa kumuhukumu mtu kwa sababu Yesu Kristu anasema msihukumu msije mkahukumiwa.”


Alisema si kusudi lake kutetea Serikali iliyoko madarakani lakini kwa habari waliyoisoma kuna tofauti kubwa kati ya mfalme Farao na Serikali nchini.


Askofu Chilongani alikosoa njia ya kufikisha ujumbe kwa Serikali akisema katika Biblia, Musa alikabiliana na Farao ana kwa ana akimtaka awaruhusu wana wa Israel waende Kanani kumuabudu Mungu au awe tayari kupokea mapigo ya Mungu.


“Ikiwa kweli Serikali iliyopo madarakani ina kasoro, kuna njia sahihi ya kupitia ili kuitaka ibadilike. Je, sisi viongozi wa dini tumeshindwa kwenda Ikulu au mahali pengine popote kukutana na viongozi wetu ambao tena ni waumini wetu hadi tukimbilie kutoa matamko. Je, huko si kuchochea vurugu.” alihoji.


Alisema kwa miaka yote viongozi wa dini huungana kutoa matamko ya pamoja panapokuwa na ulazima, hivyo kuhoji inakuaje leo kila dhehebu liwe na tamko lake.


Askofu Chilongani alisema wakati huu wa Pasaka viongozi wa dini wajipime wamepelekaje ujumbe wao wa kinabii kwa viongozi wao.


Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kibaptisti Tanzania, Michael Nhonya akihubiri katika ibada ya Pasaka mjini Dodoma jana, aliwaonya viongozi wa dini kutokuwa vyanzo vya kusababisha vurugu.


Alisema viongozi wa dini wanatakiwa kubaki kuwa walezi, washauri, wakemeaji, wenye kuonya na kuelimisha jamii ili Watanzania waendelee kuishi kwa umoja na amani.


Pia aliwatahadharisha Watanzania kutojiingiza kwenye siasa zinazoashiria uchochezi unaoweza kuleta chuki na vurugu kwa kuwa zinaweza kusababisha watu wakagawanyika.


“Viongozi wa vyama vya siasa wakae meza mmoja kwa ajili ya maridhiano badala ya kunyoosheana vidole ambavyo vimekuwa vikisababisha chuki miongoni mwa Watanzania,” alisema.


Alisema wakikaa pamoja wataweza kuondoa tofauti walizonazo.
Msimamo wa Askofu Shoo


Jana, akitoa salamu za Pasaka katika Usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo alisema hawataogopa kuitwa majina yoyote na watu wanaotaka kupotosha ujumbe uliopo katika waraka uliotolewa na maaskofu.


Alisema kuna kitu ambacho Mungu anataka kuwaambia Watanzania kupitia waraka uliotolewa na maaskofu 27 wa kanisa hilo pamoja na ule uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).


Alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo kumwandikia barua kiongozi huyo wa KKKT akimueleza kuwa ni muhimu kwa kanisa kupima kwa umakini mkubwa uzito wa kila neno kabla ya kutoa kauli kwa umma.


Profesa Kitila katika barua yake yenye kurasa sita na maneno 2,800, alisema anatoa maoni yake binafsi akiwa ni muumini wa kanisa hilo kuhusu maudhui ya waraka wa maaskofu hao 27 wa kanisa hilo uliotolewa Machi 24.


Dk Shoo bila kutaja majina, alisema baada ya waraka wa TEC na ule wa KKKT kutolewa, kuna watu wachache wameibuka wakipotosha na kupinga, huku wengine wakidai maaskofu wanasema kwa sababu sadaka zimepungua.


Februari 11, TEC ilitoa ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2018 ndani yake maaskofu wakitoa msimamo kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.


Tangu kutolewa kwa waraka wa maaskofu wa TEC na ule wa KKKT, kumekuwa na mijadala kadhaa nchini kuhusu walichozungumza viongozi hao wa dini.


Dk Shoo alisema anasikitika kwamba wanaposema jambo la ukweli linalohusu maisha ya Watanzania wote, watu wachache wanaibuka kupotosha.


“Katika waraka tuliotoa kuna watu wachache, nasema wajinga, wanasema maaskofu sasa wanasema kwa sababu sadaka zimepungua kanisani, sisi sadaka hazijapungua na Wakristo wameendelea kujitoa sana, hivyo hatujapungukiwa na kitu,” alisema Dk Shoo.


Alisema wataendelea kusema kweli na wanaotaka kuharibu ukweli huo waendelee kuharibu kwa kuwa Watanzania walio wengi, wenye hekima wanaelewa maneno yaliyozungumzwa si ya kujibiwa harakaharaka tu, bali ni ya kututafakarisha.


Alisema wataitwa majina mengi lakini wanajua ni jitihada za upotoshaji kwa ukweli uliopo katika waraka. Alisema si jambo la kawaida kwa maaskofu wa makanisa makubwa mawili nchini kukaa kwa nyakati tofauti na kutoa waraka wenye ujumbe mmoja.


“Hatukukaa na kupanga tutoe waraka lakini Baraza la Maaskofu Katoliki walikaa na kuja na waraka nasi KKKT tukakaa tukaja na waraka ukilinganisha ujumbe ni uleule. Kuna kitu Mungu anataka kutuambia kama Watanzania kupitia ujumbe ule,” alisema.


Dk Shoo alisema, “Mungu awaguse hao ambao wanatumia nguvu nyingi kutaka kupotosha, wanatumia nguvu nyingi kupaka tope ili waweze kurejea katika yale yaliyotajwa pale wakayatafakari na kama kuna hatua za kuchukua wakachukue.”


Akitoa ujumbe wa Pasaka, Dk Shoo aliwataka Watanzania kukataa nguvu zote zinazopinga uhuru, uhai, kuharibu maisha ya watu na kutia hofu kwa kuwa ufufuko wa Yesu umetoa mwanga na kuwaweka watu huru.


Alisema vitisho vya watawala vinaweza kuwafanya watoto wa Mungu wakatamani au kuendelea kukaa katika giza kutokana na hofu.


Aliwatia moyo walioelemewa na mizigo kutokana na ukandamizaji uliopo katika mifumo mbalimbali akisema Yesu amefufuka ili watu wote wawe huru.


Katika mahubiri yake, Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Kagera, Darlington Bendankheha aliwataka watendaji wa Serikali kutowanyamazisha viongozi wa dini, bali wakubali kukosolewa panapoonekana kukiukwa utaratibu wa kisheria, kiimani au kiserikali.


Imeandikwa na Florah Temba (Moshi); Sharon Sauwa (Dodoma); na Shaaban Ndyamukama (Ngara) - Mwananchi
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post