ASKOFU SHOO: WANAOPOTOSHA UKWELI WARAKA WA MAASKOFU KWA KUUPAKA MATOPE NI WAJINGA

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amesema wale wote wanaojaribu kupotosha ukweli wa waraka wa maskofu kwa kuupaka matope ni wajinga.


Askofu Shoo ametoa kauli hiyo leo katika Usharika wa Moshi Mjini Dayosisi ya kaskazini, mkoani Kilimanjaro wakati akitoa salamu za Pasaka katika ibada maalumu ya kusherekea sikukuu hiyo.

Amesema kumekuwa na baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa ambao wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kupotosha waraka wa maaskofu hao na kulipaka kanisa matope kwa malengo yao binafsi jambo ambalo halipendezi na kwamba watu hao ni wajinga.

“Wapo wanaotumia nguvu nyingi kutaka kupotosha ujumbe wa waraka wa maaskofu na wamekuwa wakilipaka kanisa matope ili waweze kurejea katika waraka ule, watu hawa naweza kuwaita ni wajinga lakini pamoja na hilo nataka wakayatafakari na kama wanaona kuna hatua za kuchukua wachukue.

“Kanisa limekuwa linapata kejeli za aina mbalimbali kutoka kwa watu hao na kuwatuhumu kuwa maskofu walifikia maamuzi ya kuandika waraka huo kutokana na sababu za kimaslahi kwa maana ya sadaka makanisani kupungua jambo ambalo si la kweli.

“Kanisa linasitikika sana, tunaposema jambo la kweli na jambo linalohusu maisha ya Watanzania wote, halafu kunatokea watu chache ambao naweza kuwaita wajinga wanakebehi na kusema eti kwa sababu sadaka zimepungua kanisani sisi sadaka hazijapungua kwani wakristo wanajitoa sana na hatujapungukiwa na kitu ila tunasema yale tunayoyaamini,” amesema.

Askofu Shoo amesema anafahamu kuwa kupitia waraka ule maaskofu wa kanisa hilo watabatizwa majina ya aina mbalimbali na kwamba hizo ni jitihada za kujaribu kuuzima ukweli ulipo katika wataka huo na wao hawajali kuhusu hilo bali watasimamia ukweli zaidi.

“Najua tutaitwa majina mengi maaskofu na hizo ni jitihada za upotoshaji wa ule ukweli ulipo katika waraka na tukumbuke hili si jambo la hivi hivi tu…. kwani kwa wakati mmoja mabaraza ya maaskofu wa makinsa makubwa mawili nchini kukaa na kutoa waraka ambao una ujumbe ulioshabihiana si kitu cha kawaida mimi nasema kuna kitu Mungu anataka kutuambia kupitia ujumbe ule tutafakari hili kama taifa,” amesema.

Na Upendo Moshi - Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527