NCHEMBA : NILITAKA SANA KUMUONA NONDO.....ACHENI KUJIFANYA MAADUI WA SERIKALI


Waziri wa Mambo ya ndani, Dk Mwigulu Nchemba amewataka wanafunzi kuachana na harakati za kutengeneza taswira mbaya kwa serikali badala yake kuwa na mitazamo chanya huku akieleza alivyotamani kumuona Nondo.

Mwigulu ameyasema hayo kwenye kongamano la UNILIFE lililofanyika Chuo cha Biashara (CBE), ambalo liliandaliwa na Mbunge wa Viti maalum Ester Mmasi, ambapo amesema alitamani kumuona mwanafunzi aliyedaiwa kutekwa hivi karibuni Abdul Nondo.

''Acheni kufanya 'Student Movement' na kujifanya maadui wa serikali, mimi nimewahi kufanya hivyo tena siku hizi zimepoa lakini sio hii ya kutaka kutengeneza picha mbaya kwa serikali, kama rafiki yangu Nondo nilitaka sana leo nimuone hapa'', amesema Mwigulu.

Aidha Mwigulu ameeleza kushangazwa na kitendo cha mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kumtaka waziri ajiuzulu, akienda mbali zaidi kwa kusema yeye alidhani anamaanisha waziri wa serikali za wanafunzi na sio yeye ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani.

Kwa upande mwingine Mwigulu amewaasa wanafunzi kuwa wema chuoni kwani kuwa kijana mwema chuoni, sio kwa kuwa kimya bali kuwa na mitazamo chanya ambayo itasaidia kujenga na kuboresha mambo mbalimbali ya serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527