ASKOFU NZIGILWA : WAKRISTO TUNATAKIWA KUJIFUNZA KUKAA KIMYA, TUONDOE VISASI NA MALUMBANO

Askofu Msaidizi wa jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa amewataka waumini kuwa na moyo wa huruma hasa katika kipindi hiki cha kukumbuka mateso ya Yesu Kristo na kuondoa malumbano ili waweze kuiona pepo.

Akihubiri katika misa ya Ijumaa Kuu jana Machi 30, iliyofanyika katika Kanisa ka Bikira Maria Mama wa Huruma, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam alisema wawe tayari kusamehe kwa wote waliowakosea na kuondoa visasi na vinyongo ambavyo vinaweza kuharibu maisha yao.

“Katika kipindi hiki cha kukumbuka mateso ya Yesu Kristo, tunapaswa kukumbuka matendo ya huruma ambayo yatazidi kutuongezea imani na kuondoa visasi na malumbano katika jamii na familia zetu.

“Wakristo tunatakiwa kujifunza kukaa kimya na kuepusha maneno na kumgeukia Kristo ili uweze kumueleza shida zako, jambo ambalo linaweza kukusaidia ukaikuta huruma yake.

“Kila mmoja anapomuangalia Yesu msalabani anapaswa kusema yesu dhambi zangu zimekuhukumu kwa sababu alikuhumiwa katika mazingira ya uonevu,” alisema.

Aidha, Askofu Nzigilwa alisema watu wanapaswa kumuonea huruma mtu anayeteseka na kamwe hawashiriki kwa ajili ya kusababisha mateso Kwa mwingine na kwamba kila mmoja anapaswa kuweka azimio la kuwa mtetezi kwa wanaoonewa na kamwe wasinyanyase mtu au kumtendea mabaya.

“Kila binadamu anateseka kwa namna tofauti ili kupimwa imani yake kama ipo imara, hivyo basi wanapaswa kuwa wavumilivu wa moyo na kumkimbilia Mungu ili iwe sehemu ya ukombozi,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527