Saturday, March 31, 2018

MAASKOFU ARUSHA WATEMA CHECHE ‘KANISA HALIWEZI KUNYAMAZISHWA AU KUFUNGWA MDOMO’

  Malunde       Saturday, March 31, 2018

UMOJA wa Makanisa ya Kikristo Mkoani Arusha jana ulisema kanisa ni chombo chenye mamlaka ya Mungu katika kukosoa, kukemea na kuelimisha waumini wake na kamwe hakiwezi kunyamazishwa na mtu yoyote. 

Akizungumza katika Ibada ya Ijumaa Kuu, Mwenyekiti wa Umoja, Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu alisema kanisa limepewa mamlaka ya kuhubiri upendo na amani hivyo hakuna atayeweza kulinyima kusema.

"Kanisa haliwezi kunyamazishwa au kufungwa mdomo. Hiki ni chombo cha kusimamia imani kwa watu wote ambao ni wakristo, wenye dini na wasiokuwa na dini hivyo haiwezi kutokea chombo ambacho kinaweza kulizuia kanisa kuzungumza au kuongea," alisema Askofu Lebulu.

Askofu huyo alisema palipokuwa na chuki, giza na hofu Mungu amelielekeza kanisa kuhubiri amani na upendo kwa wakristo duniani.

"Hivyo kama sisi tulio katika umoja wa makanisa tumwombe Mungu kuwafariji wote wanaopitia katika kipindi kigumu," alisema.

Alisema Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwasha mwenge wa Uhuru katika Mlima Kilimanjaro kama ishara ya kuangaza mwanga na nuru nchini hivyo viongozi wanatakiwa kuangaza mwanga kwa watu wote wenye hofu.

"Wakristo tunapaswa kuangaza nuru na mwanga ili kuleta upendo, amani, haki, usawa na mshikamano kwa wakristo tunaowaongoza, hivyo pale shida na matatizo yanapotokea tunatakiwa kanisa kusimama imara na kukemea bila kuangalia sifa na cheo cha mtu," alisema Askofu mstaafu Lebulu.

Alisema kuwa Kristo amewataka wakristo kuwa vyombo vya amani na upendo ambapo alieleza kwamba pale ambapo kunatokea mvurugano katika nchi na jamii kwa ujumla, Mungu amesisitiza kanisa lisimamie upatikanaji wa haki na upendo.

"Tunachosisitiza siku ya leo (Ijumaa Kuu) Kristo ameshinda mauti na ufufuo umepatikana kwa wale wenye imani. Ndiyo maana tunaweza kutamka mbele ya Mungu na binadamu kuwa Mungu ametenda miujiza."

Naye Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu aliwataka wananchi kuilinda amani na kuishi kwa upendo na kuachana na vitendo vya chuki.

Alitoa kauli hiyo wakati wa mahubiri ya Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika ushirika wa Ipagala mjini Dodoma.Kinyunyu alisema watu wote wanapaswa kuilinda amani na kuishi kwa kupendana pamoja na kusaidiana katika jamii nzima kwenye mazingira yao bila ubaguzi.

"Kristo aliupenda ulimwengu na ndiyo maana akautoa uhai wake kwa ajili yetu sisi wenye dhambi ili tukombolewe, tuwe huru na dhambi hivyo huo ni upendo wa agape aliotupenda," alisema Askofu Kinyunyu.

Alisema upendo unatakiwa kuanzia kwenye familia wanazoishi kwa kuwapenda ndugu, watoto pamoja na wote wanaowazunguka.

Aliongeza kuwa kifo cha Yesu msalabani ilikuwa ni upendo wa kipekee kwani alikubali kufa kwa ajili ya wengine ili wapate ukombozi.

Aidha, alisema wakati wote watu wanatakiwa kuilinda amani iliyopo ili kuwa na uhuru wa kuabudu na kufanyakazi za kuzalisha mali.

KUHOJI WATUHata hivyo, alisema maisha ya Yesu Kristo alipokuwa akihubiri duniani alisisitiza amani kwa watu wote kwa sababu alijua bila amani hakuna mafanikio.

Naye Mhashamu Askofu Evarist Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, alisema kipindi cha pasaka ni kipindi cha kuhoji kama watu wanaishi pamoja na Mungu na kama matendo yanakuwa na uwezo wa utendaji wa Mungu.

Alisema mwaka huu Maaskofu wa Tanzania wameleta mambo matatu ambayo aliyataja kuwa ni shukrani kwa Mungu na kuona wale walioamini kuwa wapo pamoja na Kristo.

Katika matangazo ya moja kwa moja ya televisheni kupitia kituo cha TBC1, Askofu Chegula alisema wazo lingine ni maaskofu na waumini ambao waliketi na kutathmini maisha yao kama kweli wanaishi na Kristo.

"Kutokana na mawazo ya maaskofu wetu wakati ule walivyokaa kutathmini maisha yao, kila mmoja anawajibu wa kumsahihisha mwenzake," alisema.

Alisema kila muumini ana wajibu wa kuleta ukombozi kwa wenzake, wajibu wa kusahihisha wenzake na kwenda pamoja wa wenzao.

"Huwezi ukasema wewe ni mkristo ukabaki peke yako na huna uchungu wa kuona wengine hawafuati mafundisho ya dini," alisema.

Alisema wazo la pili linawakumbusha kwamba licha ya kuwaombea mapadri, waumini wawaombee vijana ili wengi waingie kwenye utawa na upadri.

Alisema neno la tatu ambalo maaskafu na waumini waliliona ni hali halisi ya Tanzania kisiasa na kijamii.

"Umezoea mara nyingi kufikiria kwamba maaskofu wanapotoa ujumbe unamlenga labla mtu fulani, unalenga wale watu ambao ni wanafiki, watu ambao wanajidai ni wakristo lakini hawana misimamo ya kikristo ili waweze kubadilika," alisema na kuongeza:

"Ujumbe wa mwaka huu tunapoongea mambo ya kisiasa tunasema tuangalie kulialia tu kama zamani, wanasema tufikiri kabla kutenda kitu, sisi maaskofu tumeona udhaifu wetu ni huu (udhaifu wa mimi na wewe) kila mara baada ya uchaguzi ndio tunaanza kumthamini mtu je ataweza?

"Sasa mwaka huu kwa ujumbe wetu tumesema wakristo wote katika jumuiya zetu ndogondogo muanze kufikiri watu gani mwaka unaokuja tutawachagua; siyo chama fulani, watu wenye tabia fulani, lazima tujue tunataka nini, maendeleo ya namna gani, tunataka amani.

"Tunataka haki, lazima katika jumuiya ndogondogo tuwe tayari tumeonyesha kwamba watu na namna hii wapo kwenye nafasi zetu na pale watakapokuja kujiandikisha kwamba wanataka kupigiwa kura kuwa madiwani au viongozi tujue tutamchagua mtu wa aina gani."

Alisema maaskofu hawajasema kwamba sasa ni wakati wa kuchagua watu wa chama fulani kwa sababu kwa kufanya hivyo ni kuingia katika shimo lile lile la kuchagua mawazo ya watu fulani ambao hawaendani na matarajio ya wananchi.

Alisema kila jumuiya ndogondogo, kila parokia wakae na mapadri wao watathmini waumini wao nani au wa aina gani atakayekuwa kiongozi ili waweze kutimiza Azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 70, kwamba kila mmoja lazima aishi kwa amani, akifanyiwa na kutendewa haki na kuwa na amani.

"Tumeshuhudia kila mara baada ya uchaguzi tunakimbizana kama sungura... hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba kila tunavyochagua hatuchagui mtu anayeweza kutusaidia," alisema Askofu Chengula.

"Tuna mambo yetu sisi, tunafikra zetu, tunataka chama fulani ndio kiongoze, badala ya kufikiria wale waliochaguliwa wawe na lengo moja tu kutufanya sisi tupate haki zetu na kuishi kwa amani.

"Hakuna maana tufurahie watu fulani tuliowachagua lakini tunaishi katika hali ya wogawoga.

"Tunaanza uchaguzi mwaka kesho kwa sababu wote hawa hawakujiweka wenyewe, mimi na wewe ndio tuliowaweka, tuliwachagua na tuwe pamoja nao katika sala.

"Tuwe pamoja nao katika yale mazuri wanayotuonyesha ili watakaokuja na wenyewe wawe na uwezo wa kuendeleza."Sisi tunavyochagua, tusichague wale wenye roho ya ubinafsi ili tuweze kujenga nchi yetu. Wanangu sisi hatuna ubaya na mtu yoyote, mwongozo ule, ujumbe ule (Waraka wa Maaskofu Katoliki) tumeutoa kwa kujiangalia wote.

"Tuanze kujiandaa mwaka 2019 (Serikali za Mitaa) tuchague watu ambao tunaweza kuwakosoa kwa sababu binadamu hana ukamilifu wa kufikiri lakini kwa vyovyote vile hatutarudia makosa.

"Tumejitahidi kadiri ya udhaifu wetu, tumeona watu wa tabia hii, watu wa mtindo wa maisha kama hayo hao ndiyo wanaoweza kuwa viongozi wetu."

Aliwaeleza waumini hao kuwa baada ya ibada hiyo kila mmoja aende kusimulia huko anakokwenda, kwa sababu ni vita ya wote kwani wakipatikana viongozi wabaya wananchi wote wataumia.

Askofu huyo aliyekuwa akihubiri katika Ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima Parokia ya Mtakatifu Feansisco wa Asizi, Mwanjelwa jimbo la Katoliki Mbeya.

"Tukipata viongozi wazuri tutapata faida wote," alisema zaidi Askofu Chengula.

"Kila mmoja awe na kiu ya kuiona Tanzania hii iwe na upendo na mshikamano kati yetu, tunapokuja (madhabahuni) kubusu msalaba kila mmoja amnong'onezee Yesu kwamba nataka Tanzania iwe na kiu kama ya kwako katika kuwapenda Watanzania."

Imeandikwa na Allan Isack, ARUSHA, Ibrahim Joseph, DODOMA na Romana Mallya, DAR

Chanzo- Nipashe
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post