TUME YA UCHAGUZI YARIDHIA KUHAMISHWA KWA VITUO 46 VYA KUPIGIA KURA KINONDONI

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeridhia kuhamishwa kwa vituo 46 vya kupigia Kura katika kata tatu za jimbo la Kinondoni zitakazofanya Uchaguzi mdogo wa Ubunge Februari 17 mwaka huu.


Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima ameeleza kuwa uamuzi wa NEC kuridhia kuhamishwa kwa vituo hivyo, umetokana na makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Kinondoni na Vyama vya siasa juu ya kuhamishwa kwa vituo hivyo vilivyokuwa kwenye nyumba za Ibada, Zahanati na maeneo ya majengo ya watu binafsi.


Amesema Tume imeridhika na uamuzi huo kwasababu hatua zilizochukuliwa ni sahihi kwa mujibu sheria na kanuni namba 21 ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambayo inaeleza kuwa ; Vituo vya Kupigia Kura havitakiwi kuwekwa katika majengo ya nyumba za Ibada, kambi za jeshi, nyumba za watu binafsi na ofisi za vyama vya siasa.


“ Tumejiridhisha kuwa baadhi ya vituo katika Kata ya Kigogo vilikuwa katika nyumba za Ibada na vingine kuwa katika maeneo yenye ufinyu wa nafasi hivyo tumeridhia vituo hivyo vihamishwe na kupelekwa katika majengo ya umma” Amesema.


Amesema kuwa baadhi ya vituo vya kupigia Kura vilivyokuwa katika majengo ya umma ikiwemo Zahanati vimehamishwa katika shule za msingi za umma zilizo katika kata hizo ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.


Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Mwananyamala Bi. Barima Omari ameeleza kuwa kata ya Mwananyamala ina vituo vya kupigia kura 65 na wapiga kura 27,589 na kuongeza kuwa vituo nane (8) vilivyokuwa katika shule ya Sekondari Kambangwa mtaa wa msisiri A vimehamishwa. Kati ya hivyo 6 vimehamishiwa katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa ya Msolomi na 2 kuhamishiwa uwanja wa kwakopa.


Naye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kijitonyama Elizabeth Minga ameeleza kuwa Kata hiyo ina jumla ya vituo vya kupigia Kura 101, kati ya hivyo vituo 22 vimehamishwa.


Akifafanua kuhusu vituo hivyo amesema vituo 6 vilivyokuwa katika shule ya Sekondari Kenton vimehamia shule ya Msingi Mapambano na vituo 5 vilivyokuwa nje ya Ofisi ya serikali ya Mtaa wa Bwawani vimehamishiwa mbele ya ofisi hiyo. 


Aidha, vituo 6 vilivyokuwa nje ya soko la Makumbusho vimehamia ndani ya Ofisi ya Meneja wa Soko hilo na vituo 5 vilivyokuwa katika Ofisi ya Serikali za mitaa kijitonyama vimehamishiwa katika shule ya msingi kijitonyama.


Kwa upande wake Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kigogo Bw. Singoro Mdegela ameeleza kuwa kata yake ina idadi ya Wapiga kura 27,000 na Vituo vya Kupigia Kura 59.


Amesema katika Kata hiyo vituo 16 vimehamishwa ambapo vituo 5 vilivyokuwa eneo la Kiwenge kwenye Msikiti wa Shiha vimehamia Uwanja wa People na Vituo 6 vilivyokuwa kwenye Zahanati ya Kigogo vimehamishiwa katika Shule ya Msingi Kigogo ili kuruhusu shughuli za matibabu kwa wagonjwa kuendelea.


Aidha, vituo 5 katika ofisi ya serikali ya mtaa wa Mkwajuni vimehamishiwa katika shule ya secondari Kigogo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527